MFUGALE:WAANDISHI TUMIENI TAKWIMU KUIBUA UHARIBIFU WA MAZINGIRA


 Na Mwandishi Wetu, DODOMA

WAANDISHI wa habari za mazingira nchini wametakiwa kuongeza nguvu katika uandishi wa habari za uchunguzi kwa kuibua shughuli zinazochochea uharibifu wa mazingira na kuongeza athari za mabadiliko ya tabianchi, hatua inayoweza kusaidia kuleta uwajibikaji na kulinda maisha ya jamii.

Mhariri Mwandamizi wa Habari za Mazingira, Deodatus Mfugale, amesema uandishi wa kina unaotumia takwimu sahihi, sheria na ushahidi unaweza kusaidia kubaini chanzo cha changamoto za kimazingira na kuwawajibisha wanaohusika.

Mfugale ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akitoa mada kuhusu habari za uchunguzi wa mazingira katika mafunzo ya wanahabari 35 kutoka mikoa ya Kanda ya Kati, yaliyoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Wanahabari ya Usaidizi wa Jamii za Pembezoni (MAIPAC), kwa ufadhili wa UNESCO.

Amebainisha kuwa maeneo mbalimbali nchini yanaendelea kukabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi kutokana na shughuli ikiwemo ukataji miti, upanuzi wa mashamba katika maeneo yaliyohifadhiwa, uvamizi wa vyanzo vya maji, uchafuzi wa mazingira, uvamizi wa maeneo ya malisho na uchimbaji wa madini usiozingatia athari za kimazingira.

“Waandishi nendeni mkaandike habari za uchunguzi kusaidia jamii ili kuifanya dunia kuendelea kuwa salama, lakini muandike kwa usahihi na mjumuisha sauti za wananchi wanaoathirika,” amesema Mfugale.

Ameongeza kuwa wanahabari wanapaswa kutumia vyanzo mbalimbali vya taarifa, takwimu na sheria za mazingira ili kuandika habari zenye ushahidi na zinazoeleza kwa kina madhara yanayowakabili wananchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa MAIPAC, Mussa Juma, amesema mwandishi wa habari za mazingira anapaswa kuandika kwa usahihi na uhuru, kuelewa kwa kina jambo analolifanyia kazi na kuhakikisha sauti za makundi mbalimbali katika jamii, wakiwemo wanawake na vijana, zinashirikishwa.

Juma amesisitiza kuwa wanahabari wanapaswa kuchunguza zaidi athari za mabadiliko ya tabianchi zinazotokana na ongezeko la joto duniani, ukame, mafuriko, kupungua kwa uzalishaji wa chakula na uharibifu wa ikolojia.

Naye Mkurugenzi wa Miradi na Uendeshaji wa THRDC, Wakili Halima Sonda, amesisitiza umuhimu wa kuwapa waandishi wa habari wanawake fursa sawa katika kufanya uandishi wa habari za uchunguzi wa mazingira.

Amesema wanawake wanahabari wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ikiwemo udhalilishaji mitandaoni na mifumo dume katika jamii, akibainisha kuwa changamoto hizo zinapaswa kupigwa vita kwa kuzingatia sheria zinazolinda haki za wanawake.

Mafunzo hayo yamewakutanisha wanahabari kutoka mikoa ya Dodoma, Singida, Mbeya, Iringa na Morogoro, ikiwa ni sehemu ya mfululizo wa mafunzo yanayotolewa na THRDC na MAIPAC kupitia mradi unaolenga kuwawezesha waandishi wa habari za mazingira kuimarisha uwezo wao katika kuchangia uwajibikaji wa kimazingira na kuongeza uelewa wa jamii.

Mafunzo kama hayo tayari yametolewa katika Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa.

Post a Comment

0 Comments

 DK. HOMERA: AWATAKA WATANZANIA KUWA NA SUBIRA KUHUSU MABADILIKO YA KATIBA