CAMFED TANZANIA YAUNGA MKONO JUHUDI ZA SERIKALI KUBORESHA SHERIA ZA NDOA


 📍Yataka watoto wa kike kulindwa dhidi ya ndoa za utotoni

Na Asha Mwakyonde, DODOMA

NDOA za utotoni na mazingira magumu yanayowakabili watoto wa kike zimeelezwa kuwa miongoni mwa changamoto zinazohitaji ushirikiano wa Serikali na wadau ili kuimarisha ulinzi, elimu na fursa za maendeleo kwa watoto hao.

Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 25, 2026 jijini Dodoma katika Ofisi za Wizara ya Katiba na Sheria zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa lisilo la CAMFED Tanzania, Anna Sawaki wakati wa ziara ya mabinti kujifunza namna Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Juma Homera, kupitia Wizara yake anavyoshughulikia changamoto za wananchi kupitia programu ya ‘Sema na Waziri’.

Anesema baadhi ya vifungu vya sheria vimekuwa vikileta changamoto katika juhudi za kuwalinda watoto wa kike huku akisema maboresho ya sheria, hususan Sheria ya Ndoa, yana umuhimu katika kuwalinda watoto wanaotoka katika mazingira magumu.

Mkurugenzi Mtendaji huyo ameeleza kuwa taasisi zinazofanya kazi na watoto hukutana na changamoto katika kuwawezesha, kutokana na baadhi ya mazingira ya kifamilia na kisheria yanayoweza kufanya hatua hizo kuwa ngumu.

“Tunajikita katika kuwawezesha watoto wa kike wanaotoka kwenye mazingira magumu, kusoma lakini pia kuwawezesha kiuchumi,” amesema.

Sawaki ameeleza kuwa ushirikiano na wadau mbalimbali, wakiwemo Plan International Tanzania na mashirika mengine ya kimataifa, umeendelea kusaidia kuwapatia watoto hao elimu na fursa za kujijenga kiuchumi.

Amesema moja ya programu zinazolenga kuwajengea watoto wa kike uwezo ni kampeni ya Girls Takeover, inayowapa wasichana fursa ya kujifunza kuhusu uongozi na kushiriki katika nafasi mbalimbali.

Aidha, amesema katika ziara hiyo mmoja wa mabinti walioshiriki amekuwa na shauku ya kujifunza zaidi kuhusu sheria na ana matarajio ya kufanya kazi katika Wizara ya Katiba na Sheria baada ya kumaliza masomo yake ya sheria.

Amesema Plan International ndilo shirika linaloendesha na kuratibu kampeni ya 'GirlsTakeover' duniani kote na hapa nchini Tanzania

limemsaidia kupata fursa ya kutembelea wizara hiyo ili kujifunza namna inavyotekeleza majukumu yake, akibainisha kuwa fursa hiyo imemjengea hamasa ya kutimiza ndoto zake.

Sawaki ameongeza kuwa wataendelea kushirikiana na Plan International kuwafikia wasichana wengi zaidi na kuwawezesha kutimiza ndoto zao katika elimu, uongozi na maendeleo ya kiuchumi.

Aidha amesema wanaunga mkono juhudi za Serikali za kuangalia maboresho ya sheria zinazohusu ndoa na haki za watoto ili kuweka mazingira bora zaidi ya kuwalinda wasichana dhidi ya changamoto zinazoweza kuathiri maisha na ndoto zao.

Amesisitiza kuwa watoto wa kike wanahitaji kupewa fursa sawa katika elimu, uongozi na maendeleo ya kiuchumi ili waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa jamii.

Aidha, amesema wanawake viongozi, akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan wanaweza kuwa mfano kwa watoto wa kike wanaotamani kushika nafasi za uongozi siku zijazo.

Kwa upande wake binti Veronica Kalinga ambaye amesomea uwakili kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la CAMFED Tanzania, alifurahishwa na namna Wizara hiyo inavyoshughukikia kutatua changamoto za kisheria kwa wananchi.

"Nimefurahi sana kumuona Waziri wa Katiba na Sheria Dk. Homera anavyopokea simu na kusikiliza kero za wananchi kupitia programu ya 'Sema na Waziri' natamani kujifunza zaidi," amesema.

Awali Dk. Homera amewataka wanawake kujiamini, kujiandaa na kujitokeza kuchukua nafasi za uongozi kuanzia ngazi za shule na vyuo hadi katika nafasi za juu za uongozi wa kitaifa.

Amesema ushiriki wa wanawake katika uongozi, wana uwezo wa kushika nafasi mbalimbali iwapo watajiandaa na kujenga uwezo wa kujiamini.

"Hata katika vyuo vikuu, wanawake wamewahi kushika nafasi za juu za uongozi, ikiwemo nafasi za urais na makamu wa rais wa serikali za wanafunzi, jambo linaloonesha kuwa uwezo wa uongozi haupaswi kuhusishwa na jinsia" ameeleza.

Ameongeza kuwa wanawake wanapaswa kuanza kujijengea uwezo wa uongozi tangu wakiwa shuleni, kwa kushiriki katika nafasi za uongozi na kujifunza namna ya kuwasiliana na watu pamoja na kujiamini wanapokuwa mbele ya hadhira.

“Ni suala la kujitoa, kujiandaa na kujiamini. Ukiwa umejiandaa vizuri, hata kama una umri mdogo, unaweza kushika nafasi kubwa ya uongozi,” amesema 

Aidha, ameeleza kuwa uwezo wa kuzungumza mbele ya watu, kuandaa hotuba na kueleza hoja kwa ufasaha ni miongoni mwa sifa zinazoweza kumsaidia mwanamke kujenga uongozi imara.

Katika hilo, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametajwa kama miongoni mwa wanawake wanaoweza kuwa mfano wa kuigwa kutokana na nafasi yake ya uongozi na namna anavyowasilisha hotuba katika Kiswahili na Kiingereza.

Post a Comment

0 Comments

TANZANIA YAENDELEA KUJIIMARISHA KATIKA USIMAMIZI WA MAAFA