Na Asha Mwakyonde, DODOMA
WIZARA ya Katiba na Sheria imesisitiza kuendelea kushirikiana na Shirika la Plan International Tanzania katika kulinda haki za wanawake na watoto, ikiwemo kupambana na ndoa za utotoni na kuwawezesha mabinti kukabiliana na changamoto za kiuchumi.
Plan International ndilo shirika linaloendesha na kuratibu kampeni ya #GirlsTakeover, duniani kote na hapa nchini Tanzania.
Akizungumza leo Septemba 25,206 wakati wa ziara ya mabinti wa Plan International chini ya kampeni ya 'Girls takeover' katika Ofisi za Wizara ya Katiba na Sheria, zilizopo Mji wa kiserikali Mtumba kujifunza namna Wizara hiyo inavyoshughukikia na kutatua changamoto za asubuhi kupitia programu ya 'Sema na Waziri'
Waziri wa Wizara hiyo Dk. Juma Homera amesema ushirikiano huo umekuwa na mchango katika kuongeza uelewa kuhusu namna Serikali inavyoshughulikia changamoto zinazowakabili wanawake na watoto.
Amesema mabinti hao wamepata fursa ya kujifunza namna wizara inavyotekeleza majukumu yake, ikiwemo kupokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi kupitia programu mbalimbali.
Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Plan International katika shughuli za uwanjani, hususan kampeni zinazolenga wasichana na katika kutoa elimu kuhusu haki zao.
Dk. Homera amesema suala la ndoa za watoto bado ni miongoni mwa changamoto zinazohitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali, huku akieleza kuwa kuna umuhimu wa kuangalia maboresho ya sheria na mifumo inayolinda haki za watoto.
“Safari hii ni ya pamoja ya kuhakikisha mtoto wa kike anatimiza ndoto zake kupitia upatikanaji wa haki,” amesema.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwawezesha mabinti kiuchumi badala ya kuwapatia ushauri pekee huku akisema changamoto za kiuchumi zinaweza kuwafanya baadhi yao kuingia katika mazingira hatarishi.
Ameongeza wizara imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo GIZ, katika kuwawezesha baadhi ya watu wenye changamoto ili waweze kujitegemea.
Ameitaka Plan International kuangalia namna ya kuwawezesha mabinti wanaokabiliwa na changamoto katika maeneo wanayoishi ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuepuka mazingira yanayoweza kuhatarisha maisha na mustakabali wao.
Katika hatua nyingine, amesema kupitia programu mbalimbali za wizara, Serikali imekuwa ikifuatilia changamoto za wananchi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo magerezani, ambako baadhi ya wanawake na watoto hukumbana na changamoto zinazohitaji msaada wa kisheria.
Amesema baadhi ya kesi zinazofuatiliwa zinaonesha umuhimu wa kuangalia mazingira ya familia na haki za wahusika wakati wa kushughulikia masuala ya kisheria.
Amesisitiza kuwa utekelezaji wa haki unapaswa kuzingatia usawa na kwamba wanawake na wanaume wanapaswa kushughulikiwa kwa misingi ya sheria bila kubaguliwa.
Ameishukuru Plan International kwa ushirikiano wake na Wizara ya Katiba na Sheria, akiahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi hiyo katika kulinda na kukuza haki za wanawake na watoto.
Kwa upande wake Mkuu wa Sera, Mkakati na ubora kutoka Shirika la Plan International, Christina Ruhinda ameeleza kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria katika kuwapatia mabinti fursa za kujifunza kuhusu uongozi, sheria na haki za watoto, ili kuwajengea uwezo wa kutetea na kudai haki zao.
Amesema ziara hiyo imewapa mabinti fursa ya kujifunza kwa vitendo, ikiwemo kuona namna Waziri wa Katiba na Sheria anavyopokea na kusikiliza changamoto za wananchi zinazowasilishwa moja kwa moja.
Mkuu huyo wa Sera, Mkakati na ubora ameeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kuwajengea mabinti uelewa na kuwaandaa kushiriki katika masuala ya sheria, haki na uongozi.
“Leo wamepata fursa ya kukaa, kusikiliza na kuangalia namna wanavyofanya kazi, hasa katika kusikiliza changamoto za wananchi,” amesema.
Ameongeza kuwa baadhi ya mabinti walioshiriki katika programu hiyo wana taaluma na uzoefu tofauti, huku mmoja akiwa anasomea sheria na mwingine akiwa amemaliza kidato cha nne na kuendelea na safari yake ya kujifunza.
Amesema lengo kubwa la ushirikiano huo ni kuhakikisha watoto, hususan watoto wa kike, wanapata haki zao kwa usawa na wanawezeshwa kufikia ndoto zao.
“Safari yetu kubwa ni kuona mtoto anapata haki zake kwa usawa, hasa mtoto wa kike akipata haki zake kama mtoto wa kiume,” amesema.
Aidha, amesema Plan International itaendelea kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria katika shughuli mbalimbali, ikiwemo kuwapatia mabinti fursa za kushiriki katika shughuli za wizara na kujifunza zaidi kuhusu sheria na haki.
Amesema ushirikiano huo utaendelea kuwa sehemu ya kuwajengea mabinti uwezo na kuwaandaa kuwa mabalozi wa haki za watoto katika jamii.
Ruhinda amefafanua kuwa uongozi wa taasisi hiyo umeendelea kusisitiza umuhimu wa wadau mbalimbali kushirikiana katika kuhakikisha watoto wanalindwa, wanapata haki zao na wanakuwa na mazingira yanayowawezesha kutimiza ndoto zao.
Naye Jenipha Lucas kutoka Shirika hilo Akizungumza baada ya kupata fursa ya kushiriki katika kampeni hiyo amesema amejifunza mambo mbalimbali kuhusu uongozi na namna ya kuendesha kampeni zinazolenga watoto.
Amesema amefurahishwa kupata fursa hiyo na kuomba programu kama hizo ziwafikie pia wasichana walioko vijijini ambao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazowafanya washindwe kuendelea na masomo.
Ameeleza kuwa baadhi ya wasichana wanamaliza kidato cha nne ambapo hukosa fursa ya kuendelea na elimu kutokana na changamoto za kifamilia na kiuchumi.
“Mtoto ambaye amemaliza kidato cha nne , wazazi wanamkatisha masomo na kumlazimisha kuolewa, hapewi nafasi ya kuendelea na masomo,” amesema.
Ameongeza kuwa changamoto za mimba za utotoni pia bado zinawakabili baadhi ya wasichana katika maeneo ya vijijini, hali inayoweza kuwakatisha masomo na kuathiri ndoto zao za maisha.







0 Comments