DK. HOMERA: MABARAZA YA ARDHI KUPEWA NGUVU KUKABILI MIGOGORO

📍Asema Serikali yataka suluhisho la kudumu

Na Asha Mwakyonde, DODOMA

SERIKALI Kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeanza kutafakari namna ya kuimarisha mabaraza ya ardhi nchini ili yaweze kuwa chombo chenye nguvu zaidi katika kutatua migogoro ya ardhi kabla haijaibua uhasama, hasara na hata kupoteza maisha.

Akizungumzia leo Septemba 25,2026 jijini hapa katika programu ya 'Sema na Waziri' Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Juma Homera, amesema hatua hiyo inalenga kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi katika migogoro ya ardhi, ikiwemo migogoro kati ya wananchi na taasisi pamoja na wakulima na wafugaji.

Ameeleza kuwa kwa sasa mabaraza ya ardhi ya vijiji, kata na wilaya yana nafasi kubwa katika kushughulikia migogoro hiyo, hivyo kuna haja ya kuangalia kama yanaweza kuongezewa nguvu ili yawe msaada zaidi kwa jamii au kuwepo utaratibu mwingine wa kupeleka migogoro hiyo moja kwa moja mahakamani.

Dk. Homera amebainisha kuwa suala hilo limepewa msukumo pia kupitia maelekezo ya Serikali, likiwemo hitaji la kuhakikisha migogoro ya ardhi na migogoro kati ya wakulima na wafugaji inatatuliwa kwa wakati.

Amesema migogoro hiyo inapochelewa kutatuliwa inaweza kuwa na madhara makubwa kwa jamii huku akitoa mfano wa tukio la Tunduru mkoani Ruvuma ambako, kwa mujibu wa maelezo yake, watu walipoteza maisha kutokana na migogoro ya wakulima na wafugaji.

“Tayari tumeshapewa maelekezo makubwa, ni kwenda kukaa na kuona namna ya kurekebisha hizi sheria ziweze kuwa zenye tija kwa jamii yetu,” amesema.

Ameongeza kuwa Wizara ya Katiba na Sheria itashirikiana na taasisi husika, ikiwemo Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, katika kuangalia namna ya kuboresha sheria na mifumo inayohusika na utatuzi wa migogoro ya ardhi.

Katika hatua nyingine, Dk. Homera ameeleza wasiwasi kuhusu baadhi ya matukio ya wananchi kutolewa katika maeneo wanayoishi kwa kuchukuliwa mali zao na kuwekwa nje.

Amesema suala hilo linapaswa kufanyika kwa kuzingatia sheria na taratibu huku akisisitiza kuwa ikiwa mtu ana haki ya kuchukua hatua, anapaswa kufuata utaratibu uliowekwa na Serikali.

“Kama amefuata taratibu ni haki yake, lakini kama hajafuata taratibu basi anapaswa kufuata sheria ambazo zimewekwa na Serikali yetu,” amesema.

Dk. Homera amesema atawasiliana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, pamoja na viongozi wa wilaya husika ili kupata ufafanuzi na kuona namna bora ya kushughulikia changamoto hiyo.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa wananchi kutotumia nguvu au kujichukulia sheria mkononi wakati wanapokabiliwa na migogoro, akieleza kuwa hatua hizo zinaweza kuvuruga amani na kuhatarisha maisha ya watu.

Amesema Wizara hiyo itaendelea kutoa elimu ya sheria kwa wananchi ili kuwasaidia kufahamu haki zao, wajibu wao na hatua wanazopaswa kuchukua wanapokabiliwa na migogoro.

Post a Comment

0 Comments

 DK. HOMERA: AWATAKA WATANZANIA KUWA NA SUBIRA KUHUSU MABADILIKO YA KATIBA