Na Asha Mwakyonde, DODOMA
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk. Juma Homera, amewataka Watanzania kuwa na subira kuhusu mchakato wa mabadiliko ya Katiba, akisema Serikali inaendelea na taratibu za ndani zinazohitajika kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa.
Dk. Homera amesema hayo leo, Septemba 25, 2025 jijini hapa katika programu ya 'Sema na Waziri' amesema suala la mabadiliko ya Katiba limewekwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hivyo Serikali itaendelea kulifanyia kazi kwa kuzingatia taratibu na matakwa ya sheria.
Amefafanua kuwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba hauwezi kufanyika bila kufuata utaratibu wa kisheria, ikiwemo kuandaliwa kwa sheria inayowezesha mchakato huo kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa.
“Tuna jambo ambalo niwaombe Watanzania wawe na subira wakati jambo hili lipo kwenye utaratibu ulio sahihi na wasiwe na mashaka. Vitu vingi vinakwenda vizuri, muda ukifika mwenye mamlaka ya nchi atatoa maelekezo,” amesema.
Kauli hiyo inakuja wakati Serikali ikiendelea na maboresho mbalimbali katika mfumo wa sheria. Kwa mfano, Wizara imesema inaendelea kupitia sheria mbalimbali ili ziendane na mahitaji ya sasa na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

0 Comments