Na Asha Mwakyonde, GEITA
JINA la biashara linaweza kuwa mtaji mkubwa unaojengwa kwa miaka hivyo bila kulindwa kisheria linaweza kupotea mikononi mwa mtu mwingine. Hilo limesababisha Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA),kuwahamasisha wafanyabiashara na wajasiriamali kutumia Maonesho ya tisa ya Madini yanayoendelea mkoani Geita kupata elimu na huduma za usajili wa biashara.
Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la BRELA kwenye maonesho hayo, Afisa wa BRELA, Salum Makuka, ameeleza kuwa wakala huo umepeleka huduma zake kwenye maonesho hayo kwa lengo la kuwafikia wananchi kwa urahisi na kuwawezesha kupata elimu pamoja na huduma za usajili papo hapo.
Amebainisha kuwa huduma zinazotolewa ni pamoja na usajili wa kampuni, majina ya biashara, nembo za biashara (trademarks), viwanda vidogo, leseni za biashara za Daraja A, pamoja na usajili na ulinzi wa bunifu kupitia hati miliki (patent).
Makuka amesema wananchi wanaofika katika banda hilo kwa ajili ya kupata huduma hawatozwi gharama za urahisishaji wa huduma, isipokuwa hulipa ada rasmi ya Serikali inayohusika na huduma wanayoomba.
“Tumeleta huduma hizi hapa ili wananchi wapate elimu na pia waweze kusajili biashara zao papo hapo. Urahisishaji wa kupata huduma ni bure, isipokuwa wananchi watalipa ada ya Serikali,” amesema Makuka.
Amefafanua kuwa usajili wa biashara ni muhimu kwa mfanyabiashara kwa kuwa taasisi mbalimbali, ikiwamo benki na taasisi za fedha, huhitaji mfanyabiashara kuwa na usajili halali anapotafuta huduma kama mikopo au kushiriki zabuni.
Makuka ameonya kuwa kuendesha biashara bila kusajili jina la biashara kunaweza kumweka mfanyabiashara katika hatari ya kupoteza haki ya kutumia jina alilolijenga kwa muda mrefu iwapo mtu mwingine atalitangulia kulisajili.
“Unaweza kuanzisha biashara kwa juhudi kubwa, lakini mtu mwingine akaja na kusajili jina hilo. Hivyo ni muhimu kuhakikisha jina la biashara limesajiliwa ili kulinda biashara yako,” amesema.
Aidha, amesema usajili wa biashara una umuhimu katika mipango ya Serikali ya kutambua sekta mbalimbali zinazochangia uchumi, ikiwamo sekta ya madini, kwa kuwa taarifa za wafanyabiashara waliosajiliwa zinaweza kusaidia katika kupanga na kutoa huduma, motisha au fursa mbalimbali za maendeleo.
Makuka amebainisha kuwa BRELA itaendelea kutoa huduma katika maonesho hayo hadi Oktoba 3, huku akiwataka wananchi kutumia fursa hiyo kupata elimu kuhusu mfumo mpya wa BRELA unaojulikana kama BOS, unaowawezesha kufanya huduma mbalimbali kwa njia ya mtandao.
Ameeleza kuwa kupitia mfumo huo, wananchi wanaweza kupata elimu ya namna ya kufungua akaunti, kuingia katika mfumo, kufanya usajili wa biashara, pamoja na kutekeleza matakwa ya kisheria, yakiwamo kuwasilisha taarifa za mwaka (annual returns) na kulipia ada za uendelezaji wa majina ya biashara.
Kwa upande wake, mfanyabiashara kutoka Nayubi Cosmetics ameeleza kuwa BRELA imemsaidia kuongeza uelewa kuhusu usajili wa biashara na nembo.
Amesema mwaka uliopita alifanikiwa kusajili jina la biashara kupitia BRELA, lakini hakuwa akifahamu kwa kina umuhimu wa kusajili nembo ya biashara.
Anaongeza kuwa baada ya kufika katika maonesho hayo mwaka huu, alipata elimu zaidi kutoka kwa maafisa wa BRELA na kusaidiwa kukamilisha taratibu za usajili zinazohusiana na biashara yake.
Kwa mujibu wa mfanyabiashara huyo, huduma hiyo imemsaidia kuelewa zaidi mahitaji ya kisheria katika uendeshaji wa biashara na namna ya kulinda jina pamoja na utambulisho wa biashara yake.
BRELA imeendelea kutoa elimu na huduma kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wanaoshiriki maonesho hayo, huku ikiwataka wananchi kutumia fursa hiyo kupata huduma na kuelewa taratibu za kisheria za kuanzisha, kuendeleza na kulinda biashara zao.

0 Comments