Mwandishi Wetu, Dodoma
WAANDISHI wa habari za mazingira nchini wametakiwa kuibua mapema mapungufu yanayoweza kuongeza madhara ya mvua kubwa za El NiƱo, badala ya kusubiri maafa yatokee ndipo kuanza kuandika.
Ushauri huo umetolewa wakati Serikali ikitoa tahadhari kuhusu uwezekano wa kunyesha kwa mvua kubwa kupita kiasi katika maeneo mbalimbali nchini kuanzia mwezi ujao, hali inayoweza kusababisha mafuriko na madhara mengine endapo hatua za maandalizi hazitachukuliwa mapema.
Akifunga mafunzo ya waandishi wa habari za mazingira kutoka mikoa ya Kanda ya Kati, yaliyoandaliwa na Taasisi ya Wanahabari ya Usadiaji wa Jamii za Pembezoni (MAIPAC) kwa kushirikiana na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), kwa udhamini wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma, amesema waandishi wana wajibu wa kuibua changamoto zilizopo kabla ya mvua hizo kuanza.
Juma anasema bado kuna mapungufu katika maeneo mbalimbali yanayohitaji hatua za haraka ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo.
Anawataka waandishi kuacha kuishia kuandika matamko ya viongozi pekee, badala yake wafanye ufuatiliaji wa kina na kuibua mambo yanayopaswa kufanyiwa kazi sasa.
“Kuna maeneo katika miji yetu bado mitaro imeziba, kuna maeneo vimetolewa vibali kujengwa nyumba au maeneo ya biashara kwenye njia za maji. Tuandike sasa ili Serikali na wadau wengine wachukue hatua,” amesema Juma.
Ameongeza kuwa kuna miradi ya ujenzi wa barabara inayoendelea, huku baadhi ya mifumo ya maji ikiwa haijaelekezwa ipasavyo na hivyo kuhatarisha makazi ya wananchi.
“Tuandike sasa ili wakandarasi waboreshe mifumo ya maji badala ya kusubiri maafa,” anasema.
Juma, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari (JOWUTA), amewataka wanahabari kufanya uchunguzi kuhusu kuibuka kwa migogoro kati ya wakulima, wafugaji na wahifadhi, ambayo katika baadhi ya maeneo imeanza kusababisha vifo.
Naye Mkurugenzi wa Miradi na Uendeshaji wa THRDC, Wakili Halima Sonda, amewataka waandishi walioshiriki mafunzo hayo kuonesha tofauti katika uandishi wao kwa kuandaa habari zitakazochochea hatua na mabadiliko katika jamii.
“Nendeni mkaandike habari za mazingira ambazo zitachochea mabadiliko ya sheria, sera, mitazamo na uwajibikaji,” amesema Wakili Sonda.
Aidha, amewataka wanahabari kuzingatia sheria na maadili ya uandishi wa habari wakati wanapotekeleza majukumu yao.
Mafunzo hayo yalishirikisha waandishi 35 kutoka mikoa ya Dodoma, Morogoro, Mbeya, Iringa na Singida.
Mafunzo kama hayo tayari yamefanyika kwa waandishi kutoka Kanda ya Kaskazini na Ziwa, huku programu hiyo ikitarajiwa kuendelea katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga na Zanzibar.




0 Comments