TPDC YAWAPA WANANCHI TASWIRA YA MIRADI YA MAFUTA NA GESI KWA TEKNOLOJIA


Na Asha Mwakyonde, GEITA

TEKNOLOJIA ya Ukweli Uhalisia (Virtual Reality) imegeuka kuwa kivutio kikubwa katika banda la Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),kwenye Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dk. Samia Suluhu Hassan, mkoani Geita, huku wananchi wakipata fursa ya kujionea kwa njia ya kidijitali namna shughuli za mafuta na gesi zinavyotekelezwa.

Kupitia teknolojia hiyo, wageni wanaotembelea banda la TPDC wanaweza kupata taswira ya shughuli mbalimbali zinazofanyika katika miradi ya mafuta na gesi, ikiwemo uchorongaji na usafirishaji wa gesi asilia, bila kulazimika kufika katika maeneo halisi ya miradi hiyo.

Akizungumza leo Septemba 28,2026 katika maonesho hayo, Afisa Masoko wa TPDC, Grace Chigugu, amesema ushiriki wa shirika hilo unalenga kuwaelimisha wananchi na wadau kuhusu majukumu ya TPDC, teknolojia zinazotumika katika sekta ya mafuta na gesi, pamoja na fursa zinazopatikana katika sekta hiyo.

Grace amefafanua kuwa TPDC inatekeleza majukumu yake ya kimkakati kuanzia katika utafiti na utafutaji wa mafuta na gesi, uzalishaji, uchakataji hadi usambazaji wa nishati hiyo kwa matumizi mbalimbali.

Ameeleza kuwa katika maonesho hayo, wataalamu wa TPDC wanatoa elimu kuhusu matumizi ya teknolojia za kisasa zinazosaidia kutambua miamba yenye viashiria vya mafuta na gesi, pamoja na mifumo ya kisasa ya uchorongaji na usafirishaji.

“Kupitia teknolojia hii ya Virtual Reality, wananchi wanapata fursa ya kujifunza na kuona kwa karibu namna shughuli mbalimbali za mafuta na gesi zinavyotekelezwa, bila kulazimika kwenda katika maeneo ambayo miradi hiyo inafanyika,” amesema Grace.

Ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia hiyo ni miongoni mwa njia zinazotumiwa na TPDC kuwafikishia wananchi elimu kwa njia shirikishi na kuwawezesha kuelewa kwa vitendo shughuli zinazofanyika katika sekta ya mafuta na gesi.

Kwa mujibu wa Grace, ushiriki wa TPDC katika maonesho hayo pia ni sehemu ya jitihada za shirika hilo kuendelea kuwafikia wananchi, wafanyabiashara na wadau wengine kwa kuwapatia taarifa kuhusu huduma, fursa za uwekezaji na maendeleo yanayopatikana katika sekta ya mafuta na gesi.

Akizungumzia manufaa ya sekta hiyo kwa Mkoa wa Geita, Grace amebainisha kuwa mkoa huo unaendelea kunufaika na miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali kupitia TPDC, ikiwemo Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), unaopita katika maeneo mbalimbali na kuchochea shughuli za kiuchumi.

Ameeleza kuwa kupitia kampuni yake tanzu ya TANIL (Tanoil), TPDC pia inamiliki na kuendesha kituo cha mafuta mkoani Geita kinachotoa huduma za nishati kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo usafirishaji na shughuli zinazohusiana na sekta ya madini.

Grace amesema Serikali inaendelea na mipango ya kupanua matumizi ya gesi asilia kwa kuipeleka katika mikoa mbalimbali ya Kanda ya Kaskazini na Kati, ikiwemo Morogoro, Dodoma, Tanga, Kilimanjaro na Arusha.

Amebainisha kuwa mipango hiyo inalenga pia kupanua miundombinu ya gesi asilia hadi katika maeneo mengine nchini, ikiwemo Mkoa wa Geita, katika miaka ijayo.

“Lengo ni kuhakikisha wananchi na viwanda vinapata nishati ya uhakika na kwa gharama nafuu, sambamba na kuchochea shughuli za uzalishaji na uwekezaji katika maeneo mbalimbali nchini,” amesema.

TPDC imeendelea kuwahimiza wananchi, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini wanaoshiriki maonesho hayo kutembelea banda lake ili kupata elimu zaidi kuhusu shughuli za shirika, teknolojia zinazotumika katika sekta ya mafuta na gesi, pamoja na fursa za uwekezaji na huduma zinazotolewa.

Post a Comment

0 Comments

TPDC YAWAPA WANANCHI TASWIRA YA MIRADI YA MAFUTA NA GESI KWA TEKNOLOJIA