Na Asha Mwakyonde, DODOMA
WAKATI Serikali ikiendelea kusisitiza utoaji wa huduma bora kwa wananchi, taasisi mbalimbali za umma zimeanza kuonesha mafanikio, ubunifu na teknolojia zinazotekelezwa katika kuwahudumia Watanzania kupitia Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma ikiwamo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),
Shirika hilo ambalo limewasilisha teknolojia ya matumizi ya gesi asilia katika sekta ya usafiri kupitia magari yanayotumia nishati hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, leo Juni 17, 2926 ameembelea mabanda mbalimbali ya taasisi za Umma likiwamk la TPDC ili kujionea huduma, miradi na ubunifu unaotekelezwa kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya Taifa.
Akitoa maelezo kwa Waziri huyo kuhusu bidhaa wanazozionesha katika maonesho hayo Mtaalamu Mwandamizi wa TPDC Hassan Temba, amesema matumizi ya gesi asilia kwenye magari yanaendelea kuwa suluhisho mbadala lenye manufaa makubwa kutokana na gharama zake kuwa nafuu zaidi kuliko mafuta ya kawaida.
Amefafanua kuwa pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa vyombo vya usafiri, nishati hiyo ina mchango mkubwa katika kulinda mazingira kwa kupunguza kiwango cha uchafuzi wa hewa unaotokana na matumizi ya mafuta.
Temba ameeleza kuwa TPDC inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu fursa zilizopo katika matumizi ya gesi asilia, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi na rafiki kwa mazingira.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yamekusanya taasisi mbalimbali za serikali na mashirika ya umma, yakitoa fursa kwa wananchi kupata elimu, huduma na taarifa kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa kwa ajili ya maendeleo ya nchi na ustawi wa wananchi.

0 Comments