RIDHIWANI ARIDHISHWA NA UTENDAJI WA EWURA, APONGEZA UKARIBU WA HUDUMA KWA WANANCHI

Na Asha Mwakyonde, DODOMA

JITIHADA za Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) katika kusimamia sekta za nishati na maji pamoja na kusogeza huduma karibu na wananchi zimeendelea kutambuliwa, baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, kuipongeza mamlaka hiyo kwa utendaji wake unaolenga kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.

Ridhiwani ametoa pongezi hizo leo Juni 17, 2026, alipotembelea banda la EWURA katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.

Akiwa katika banda hilo, Waziri huyo alipata maelezo kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na EWURA pamoja na namna mamlaka hiyo inavyoshughulikia changamoto za wananchi katika sekta za nishati na maji.

Baada ya kupokea taarifa hizo, amesema ameridhishwa na utendaji wa EWURA na juhudi zake za kuhakikisha huduma zinazodhibitiwa na mamlaka hiyo zinawafikia wananchi kwa ufanisi na kwa wakati.

“Hongereni sana kwa kazi kubwa mnayoifanya,” amesema Waziri Ridhiwani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa EWURA, Hawa Mniga, amesema ushiriki wa mamlaka hiyo katika maadhimisho hayo unalenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake pamoja na kupokea na kutatua kero mbalimbali zinazohusiana na huduma za nishati na maji.

Ameeleza kuwa wananchi wanaotembelea banda la EWURA wanapata nafasi ya kujifunza kuhusu huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo, kuuliza maswali na kuwasilisha changamoto zao ili zipatiwe ufumbuzi kwa haraka.

“Tupo hapa kuwafikia wananchi moja kwa moja kwa kuwapatia elimu kuhusu huduma zetu, kupokea kero zao na kushughulikia migogoro inayohusiana na masuala ya nishati,” amesema Mniga.

Ameongeza kuwa maadhimisho hayo ni fursa muhimu kwa EWURA kuendelea kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu haki na wajibu wao katika sekta zinazodhibitiwa na mamlaka hiyo, huku ikikusanya maoni yatakayosaidia kuboresha zaidi utoaji wa huduma kwa jamii.

Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2026 yalianza Juni 16 na yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 25, yakihusisha taasisi mbalimbali za umma zinazowasilisha huduma na mafanikio yao kwa wananchi.

Post a Comment

0 Comments

MKURUGENZI WA UCHAGUZI APONGEZA UFANISI NA UWAZI WA MFUMO WA UAGIZAJI MAFUTA KWA PAMOJA