REA YAONESHA MFUMO WA KIDIGITALI WA UFUATILIAJI UMEME, RIDHIWANI AKABIDHIWA JIKO LA NISHATI SAFI KATIKA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA


Na Asha Mwakyonde, DODOMA

WANANCHI sasa wanaweza kufuatilia hali ya upatikanaji wa umeme katika vijiji na vitongoji mbalimbali nchini kwa urahisi zaidi kupitia mfumo wa kidijitali ulioanzishwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), hatua inayolenga kuongeza uwazi na kurahisisha upatikanaji wa taarifa za huduma hiyo muhimu.

Mfumo huo ulielezwa kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, alipotembelea banda la REA katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma.

Akitoa maelezo leo Juni 17,2926 Afisa Upimaji Mwandamizi wa REA, Hussein Shambas, amesema mfumo huo unaonyesha maeneo yote yaliyopata umeme, yasiyopata huduma hiyo pamoja na yale yaliyopo katika mpango wa kuunganishiwa umeme.

Amesema teknolojia hiyo inamwezesha mwananchi kupata taarifa za kina kuhusu hali ya upatikanaji wa umeme moja kwa moja kupitia simu yake ya mkononi, jambo linaloongeza uwazi katika utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini.

Shambas ameeleza kuwa REA imeendelea kupata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme, ambapo hadi sasa vitongoji 39,840 sawa na asilimia 77 ya vitongoji vyote nchini vimeunganishiwa umeme.

Ameongeza kuwa vitongoji 12,736 vilivyosalia vinatarajiwa kufikiwa na huduma hiyo ifikapo mwaka wa fedha 2030/2031.

Katika kuonesha uwezo wa mfumo huo, alimwongoza Waziri Kikwete kupitia takwimu za Mkoa wa Pwani, Wilaya ya Bagamoyo, Jimbo la Chalinze, ambapo vitongoji 286 tayari vina huduma ya umeme, vitongoji 133 vikiwa katika mpango wa kuunganishiwa umeme na vitongoji 50 vikiwa katika hatua za utekelezaji wa miradi.

"Mfumo huo una uwezo wa kutoa taarifa za kina hadi ngazi ya kitongoji, ikiwemo maeneo yaliyounganishiwa umeme na yale yanayosubiri kufikiwa na huduma hii," amesema.

Katika hatua nyingine, REA imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kumkabidhi Waziri Kikwete jiko la umeme lenye plate mbili ili awe balozi wa kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi katika kuhifadhi mazingira na kuboresha afya za wananchi.

Post a Comment

0 Comments

FCC YAIMARISHA ELIMU YA USHINDANI NA ULINZI WA WALAJI