MKUU WA WILAYA YA DODOMA ATOA WITO WA ELIMU YA USALAMA BARABARANI KWA WAENDESHA BODABODA


 Na Asha Mwakyonde, Dodoma

MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri, ametembelea banda la Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), katika Maonesho ya Wakulima Kitaifa ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma, na kutoa wito kwa MOI kushirikiana na taasisi na vyama mbalimbali katika kutoa elimu ya usalama barabarani kwa waendesha bodaboda ili kusaidia kupunguza ajali.

Akizungumza leo, Jumatano Agosti 6, 2025, katika banda hilo, Mhe. Shekimweri ameipongeza MOI kwa kazi kubwa inayofanya katika kutoa huduma za kibingwa na kibobezi kwa wahanga wa ajali, huku akiisisitiza taasisi hiyo kutumia utaalamu wake pia kwa kutoa elimu ya kinga kwa jamii.

"Nawapongeza MOI kwa kazi nzuri mnayofanya, lakini pia nawasihi mshirikiane na taasisi kama VETA na vyama vya waendesha bodaboda kama UWAMIDO ili kuwafikia kwa wingi na kuwapatia elimu ya usalama barabarani. Hii itasaidia kupunguza ajali na ulemavu unaotokana na uzembe au kutokuzingatia sheria," alisema Mhe. Shekimweri.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya alipendekeza kufanyika kwa ziara maalum za waendesha bodaboda kutembelea wagonjwa waliolazwa MOI kutokana na ajali za barabarani ili kujifunza kwa vitendo madhara ya ajali na hivyo kuchukua tahadhari zaidi.

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Radiolojia kutoka MOI, Dkt. Angela Isangya, alimhakikishia Mhe. Shekimweri kuwa taasisi hiyo iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali katika juhudi za kuzuia ajali kwa kutoa elimu ya kinga na usalama barabarani.

Maonesho ya Nanenane mwaka huu yanaendeshwa chini ya kaulimbiu isemayo "Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025," na yanatarajiwa kufikia kilele chake Agosti 8, 2025 katika Viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma.


Post a Comment

0 Comments

MATIVILA AAGIZA MKANDARASI KUFANYA KAZI USIKU NA MCHANA