DC KONDOA AFURAHISHWA NA HAMASA YA KILIMO CHA MKONGE NANE NANE


Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MKUU wa Wilaya ya Kondoa, Mhe. Fatma Nyangassa, ameeleza kufurahishwa na hamasa inayofanywa na Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), ambayo imesaidia kupatikana kwa wakulima zaidi ya 15 wenye jumla ya ekari takriban 240 za zao la mkonge ndani ya muda mfupi.

Akizungumza leo, Jumatano Agosti 6, 2025, alipotembelea banda la TSB katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, Mhe. Fatma aliipongeza TSB kwa juhudi hizo, huku akitaka kujua hali ya uzalishaji wa mkonge kitaifa, hali ya Mkoa wa Dodoma, pamoja na mkoa unaoongoza kwa uzalishaji. Aidha, alieleza matarajio yake kuona Mkoa wa Dodoma, hususan Wilaya ya Kondoa, ukiwa kinara wa uzalishaji wa zao hilo.

Akitoa taarifa kwa Mhe. Fatma, Mkuu wa Sehemu ya Maendeleo ya Mkonge wa TSB, Bw. Simon Kibasa alisema kuwa bado uzalishaji wa mkonge haujaanza kwa kiwango kikubwa katika Mkoa wa Dodoma, kutokana na wakulima wengi kuwa katika hatua za awali za kilimo.

Amesema hadi sasa, uzalishaji wa mkonge nchini umefikia tani 61,215 kutoka tani 39,484 mwaka 2021. Mkoa wa Tanga unaongoza kwa uzalishaji huo, ukiwa na zaidi ya tani 34,000 kwa mwaka.

“Tunategemea uzalishaji utaendelea kuongezeka kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wakulima katika kipindi cha hivi karibuni. Kwa Mkoa wa Dodoma, wakulima wengi bado hawajaanza kuvuna mkonge wao kwa kuwa wameanza kilimo hicho karibuni, baada ya serikali na bodi kuendesha kampeni ya uhamasishaji ambayo imepokelewa vizuri na wananchi,” amesema Kibasa.

Ameongeza kuwa hadi sasa, Mkoa wa Dodoma una zaidi ya ekari 240 za mkonge kutoka kwa wakulima waliokwisha tembelewa, na kuna wengine ambao bado hawajafikiwa na bodi. “Kupitia maonesho haya, wakulima watatu walifika jana na kuomba kutembelewa ili wasajiliwe. Tutaenda kuwatembelea mara tu baada ya maonesho haya kumalizika,” ameongeza.


Post a Comment

0 Comments

MATIVILA AAGIZA MKANDARASI KUFANYA KAZI USIKU NA MCHANA