SELF MF YAWEZESHA WAKULIMA ,VIJANA MIKOPO YENYE MUDA RAFIKI WA MAREHESHO

Na Asha Mwakyonde, DODOMA 

MENEJA Masoko na Uhamasishaji kutoka mfuko wa SELF Microfinance Fund, Linda Mshana ameeleza kuwa mikopo ya Self Microfinance imebuniwa kuendana na mazingira ya kijamii na kiuchumi ya walengwa, hasa kwa kuzingatia msimu wa shughuli husika ili kuwaepusha wateja na ugumu wa marejesho.

Akizungumza leo Agosti 4,2025 katika Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Kitaifa 'Nane nane' yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni Jijini hapa, amesema

wanazingatia kalenda ya shughuli za mteja huku akitolea mfano kwa mkulima ambaye atalipa kulingana na msimu wake wa mavuno. 

Meneja huyo amesema hiyo inawasaidia wateja wao kutokuwa na presha ya kulipa kabla hawajapata mapato.

Linda ameongeza kuwa lengo la ushiriki wao kwenye maonesho hayo ni kuwasogezea wananchi huduma za kifedha, hasa mikopo ya maendeleo, pamoja na kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya fedha na bima ya mazao.

Amesema wanatoa mikopo kwa wakulima, wavuvi, wafugaji, wajasiriamali, na hata wafanyakazi wa taasisi za umma na binafsi wanaotoa huduma za kifedha. 

"Tupo katika maeneo mbalimbali ya maonesho ya Nanenane Dodoma, Morogoro, Mwanza na Lindi kwa ajili ya kutoa huduma hizi,” alisema Linda.

Meneja huyo amesema katika hatua nyingine, Self Microfinance imewahamasisha vijana kote nchini kuchangamkia fursa ya mikopo kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha kisasa, ikiwemo uboreshaji wa mbegu, ununuzi wa pembejeo, vifaa vya umwagiliaji na teknolojia bora za kilimo.

“Tuna mikopo maalum kwa ajili ya vijana. Tunataka kuona vijana wanabadilisha mtazamo kuhusu kilimo, kutoka kilimo cha mazoea hadi kilimo cha kibiashara,” amesema.

Amefafanua kuwa moja ya mfano halisi wa mafanikio ya vijana kupitia mikopo ya Self ni mradi wa “Kahawa Mkononi”, unaoendeshwa na kijana Faustine Masanja.

Kwa upande wake Faustine amesema mradi wake ulianzishwa kupitia msaada wa Self Microfinance, kwa ushirikiano na Wizara ya Kilimo kupitia programu ya BBT (Building a Better Tomorrow), na Bodi ya Kahawa Tanzania.

“Tulikutana na watu kutoka Bodi ya Kahawa na Wizara ya Kilimo, walituelekeza namna ya kuanzisha biashara hii, na kutuunganisha na Self Microfinance. Kupitia mkopo huo, niliweza kufungua duka la kuuza kahawa na sasa nauza kahawa kwa njia ya kisasa,” amesema Faustine.

Ameeleza kuwa mradi huo umeleta mabadiliko makubwa kwa vijana, kwani si tu unaongeza kipato, bali pia unawawezesha kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa nchi.

“Tunapongeza Wizara ya Kilimo, Bodi ya Kahawa na Self Microfinance kwa kuona umuhimu wa kuwashika mkono vijana. Tunawaomba vijana wengine wasikate tamaa, wajiorganize, wachangamkie fursa hizi,” alisema.

Mfuko wa Self Microfinance Found ni taasisi ya kifedha ambayo ipo chini ya Wizara ya Fedha, imeeleza dhamira yake ya kuwawezesha Watanzania kiuchumi kupitia utoaji wa mikopo nafuu kwa makundi mbalimbali ya kijamii, ikiwemo wakulima, wavuvi, wafugaji, wafanyabiashara na vijana wanaojihusisha na shughuli za uzalishaji.

Post a Comment

0 Comments

MKUU WA WILAYA YA DODOMA ATOA WITO WA ELIMU YA USALAMA BARABARANI KWA WAENDESHA BODABODA