Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi salama na sahihi ya ndege nyuki (drones) katika shughuli za kilimo, ikiwa ni sehemu ya ushiriki wake katika Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa mtaalam kutoka TCAA, teknolojia ya ndege nyuki inazidi kuwa nyenzo muhimu katika kilimo cha kisasa, ikitumika katika upuliziaji wa dawa, ufuatiliaji wa afya ya mazao, uchambuzi wa udongo, na hata utunzaji wa kumbukumbu za mavuno kwa usahihi mkubwa.
Akizungumza katika banda la TCAA, Mkaguzi wa Ndege Nyuki kutoka TCAA Bw. Ibrahim Abdalah alisema Matumizi ya Ndege Nyuki katika kilimo yameleta mapinduzi makubwa, lakini ni muhimu yaendane na kanuni za kiusalama na usajili.
"TCAA tunahakikisha matumizi haya yanafanyika kwa ufanisi bila kuhatarisha usalama kwa wote wanaotumia anga," alieleza Abdalah.
Kwa mujibu wa Abdalah TCAA imesisitiza kuwa kila ndege nyuki inapaswa kusajiliwa rasmi na kuruhusiwa kutumika kwa mujibu wa Sheria ya Usafiri wa Anga na miongozo ya matumizi ya ndege nyuki .
Kwa kutambua nafasi ya teknolojia hii katika maendeleo ya kilimo na uchumi, TCAA inatoa wito kwa wakulima, watafiti na watoa huduma za kilimo kutumia ndege nyuki kwa kufuata taratibu na kuwasiliana nao wakati wowote ili kupata ushauri, msaada wa kiufundi na kufahamu namna ya kupata vibali stahiki kwa matumizi halali ya ndege nyuki nchini.
0 Comments