Na Asha Mwakyonde, DODOMA
MKUU wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Mkoa wa Dodoma, Deodatus Orota, amesema kuwa chuo hicho kimefanikiwa kuwafikia wanawake 780 kutoka taasisi ya Wanawake na Samia kupitia programu mbalimbali za mafunzo zinazotolewa kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi.
Akizungumza leo, Agosti 5, 2025, katika Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Kitaifa yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Orota amesema lengo ni kuwafikia wanawake wapatao 3,000 katika mkoa huo kupitia mafunzo ya ufundi stadi.
Ameeleza kuwa wanawake hao wamenufaika na mafunzo ya vitendo kupitia chuo hicho, ambapo baadhi ya kozi walizopatiwa ni ususi, usafi, upishi, ushonaji na huduma kwa wateja.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wanawake na Samia Taifa, Fatma Madidi, amesema zaidi ya wanawake 10,000 wameshapata mafunzo kutoka vyuo vya VETA 80 vilivyopo Tanzania Bara.
Amesema wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fursa ya mafunzo hayo kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore.
“CPA Kasore aliona umuhimu wa kuwawezesha wanawake ili waweze kujitegemea kupitia mafunzo haya ambayo yatawasaidia kuajiriwa au kujiajiri na hatimaye kuwaajiri wengine,” amesema Madidi.
Ameongeza kuwa Wanawake na Samia ni umoja unaomuunga mkono Rais Samia kwa vitendo, na kwa sasa wanafanya hivyo kupitia kushiriki kikamilifu katika mafunzo yanayotolewa na VETA nchi nzima.
Naye Ester Kimweri, Mwenyekiti wa Hamasa kutoka Wanawake na Samia Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Hamasa Taifa, amesema wamefaidika kwa kiasi kikubwa na mafunzo hayo, na sasa wanazalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo pilipili, sabuni, mikate na biskuti kwa ajili ya soko.
0 Comments