Na Asha Mwakyonde, DODOMA
MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Profesa Sifuni Mchome, amesema kuwa VETA imejipanga kuhakikisha Watanzania wa ngazi mbalimbali wanapata elimu na mafunzo ya ufundi ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kuchangia maendeleo ya taifa.
Akizungumza leo Agosti 7,2025 wakati wa ziara yake katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yanayofanyika jijini Dodoma, kwenye banda la Mamlaka hiyo Profesa Mchome amesema mafunzo yanayotolewa na VETA yanalenga kuwasaidia wananchi kujiajiri, kuajiriwa na kuchangia maendeleo ya maeneo yao na taifa kwa ujumla.
"VETA ni ya kila mtu. Leo nimetembelea banda letu ili kujionea shughuli mbalimbali zinazofanyika katika maonesho haya ambayo hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuonyesha mafanikio ya maendeleo katika sekta mbalimbali," amesema Profesa Mchome.
Amebainisha kuwa VETA imepiga hatua kubwa katika ubunifu, na kwamba baadhi ya ubunifu unaoonyeshwa unahusisha matumizi ya nishati ya umeme. Aliahidi kuwa katika maonesho yajayo kutakuwa na ubunifu zaidi unaogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Profesa Mchome amewataka wadau mbalimbali kushirikiana na VETA katika kuzalisha kwa wingi bidhaa na huduma zinazotokana na ubunifu wa wanafunzi na walimu wa vyuo vya ufundi, ili ziweze kuwafikia wananchi kwa matumizi mapana.
"Kama taifa tunapaswa kuwa na uchumi bunifu unaozalisha kwa kiwango cha juu. Ili kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, ni lazima tuwekeze katika elimu ya ufundi na ujuzi, na VETA ina mchango mkubwa katika mchakato huu," amesisitiza.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Rosemary Senyamule, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kufungua fursa nyingi za kiuchumi, hasa kwa wanawake, lakini akabainisha kuwa bado wanawake wengi hawajazitumia ipasavyo.
"Tunayo vyuo vya VETA lakini je, wanawake wangapi wanatambua umuhimu wa elimu ya ufundi? Ni muhimu wanawake kuchukua hatua ya kujifunza ili wajikomboe kiuchumi," amehoji Senyamule.
Aidha, ametoa pongezi kwa Mkurugenzi Mkuu wa VETA kwa kuridhia wanawake kupata fursa ya elimu ya ufundi na ujuzi unaoweza kubadilisha maisha yao, huku akitoa wito kwa wanawake wote nchini kuitumia fursa hiyo adhimu.
"Ufundi ni ujuzi unaokupa maarifa kwa haraka ya kuweza kufanya kazi na kupata faida. Fursa bado ipo, ni juu ya wanawake kuzitumia kwa maendeleo yao binafsi na taifa kwa
ujumla," ameongeza.
0 Comments