PURA: USHIRIKIANO WA SEKTA YA GESI ASILIA NA KILIMO KUONGEZA TIJA YA KIUCHUMI

Na Asha Mwakyonde, DODOMA

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni, amesema kuwa sekta ya gesi asilia na sekta ya kilimo ni nyanja zinazotegemeana kwa karibu, na kwamba ushirikiano wa karibu kati ya sekta hizo unaweza kuongeza tija na kuchochea maendeleo ya uchumi wa nchi.

Mhandisi Sangweni aliyasema hayo leo Agosti 7, 2025, alipotembelea Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane yanayoendelea kufanyika jijini Dodoma.

Akizungumzia fursa zilizopo, Sangweni ameeleza kuwa gesi asilia inayozalishwa nchini inaweza kutumika kama malighafi ya kutengeneza ammonia kemikali muhimu inayotumika kuzalisha mbolea aina mbalimbali, ikiwemo urea.

Aidha, amefafanua kuwa matumizi ya gesi asilia kwenye magari yamechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za uendeshaji. Ameongeza kuwa endapo gesi hiyo itatumika katika magari yanayosafirisha mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, itasaidia kupunguza gharama za usafirishaji na kuongeza faida kwa wakulima na wafugaji.

Katika upande mwingine, Mkurugenzi huyo amesisitiza kuwa sekta ya kilimo imekuwa nguzo muhimu katika utekelezaji wa miradi ya mafuta na gesi asilia, hasa kwa kutoa huduma ya chakula kwa wataalamu wanaoshiriki katika miradi hiyo.

Hata hivyo, ametaja changamoto ya uhitaji wa bidhaa za kilimo zenye viwango vya ubora vinavyokubalika kimataifa, hususan na kampuni za nishati za kimataifa.

 Amesema kuwa ni wachache kati ya watoa huduma wazawa wanaoweza kukidhi viwango hivyo.

Licha ya changamoto hizo, PURA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha viwango na ubora vinavyohitajika vinafikiwa, kwa lengo la kukuza ushiriki wa Watanzania na kuinua uchumi wa taifa kwa ujumla.



Post a Comment

0 Comments

Mgomba wa Chama cha National League for Democracy (NLD),Doyo Hassan Doyo akiingia na usafiri wa bajaji  MC 816 CNUkuchukua fomu ya urais 2025.