WANANCHI NA WAWEKEZAJI WAASWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA ZAO LA MKONGE ILI KUJINUFAISHA


Na Asha Mwakyonde, DODOMA

MKUU wa Sehemu ya Maendeleo ya Mkonge kutoka Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Simon Kibasa, ameeleza kuwa sekta ya mkonge kwa sasa imeimarika kibiashara ambapo inatoa fursa nyingi za uwekezaji.

Pia amewataka Wananchi na wawekezaji nchini wametakiwa kutumia kikamilifu fursa zinazochipuka katika sekta ya mkonge, kufuatia kuongezeka kwa mahitaji ya mbegu bora, mitambo ya usindikaji, na bidhaa za thamani zinazotokana na zao hilo linalorejea kwa kasi sokoni.

Wito huo umetolewa leo Agosti 7,2025 wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yanayofanyika jijini Dodoma, ambapo alibainisha kuwa kwa sasa, mahitaji ya mbegu za mkonge kitaifa ni zaidi ya milioni 60, wakati uwezo wa sasa wa uzalishaji uko chini ya milioni 25.

Ameeleza kuwa hiyo inaonesha kuna pengo la zaidi ya mbegu milioni 35, ambalo linaweza kuzibwa na wawekezaji wapya,” alisema Kibasa.

Kibasa amesema kuwa mafanikio ya sekta hiyo yanaonekana pia kwenye takwimu, ambapo uzalishaji wa mkonge umeongezeka kutoka tani 39,000 mwaka 2020 hadi kufikia tani 61,000 mwaka 2024. 

Aidha, idadi ya wakulima imeongezeka kutoka 7,551 hadi zaidi ya 20,000 ndani ya kipindi hicho huku akisema licha ya jitihada za serikali katika kuwezesha mitambo ya usindikaji wa mkonge, bado kuna upungufu wa zaidi ya mitambo mikubwa 25 ya kisasa, hivyo kutoa nafasi kwa sekta binafsi kuwekeza na kusaidia kuongeza mnyororo wa thamani wa zao hilo.

Kibasa amezitaja fursa nyingine kuwa ni pamoja na biashara ya singa za mkonge kwa ajili ya masoko ya ndani na nje ya nchi, pamoja na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali zenye thamani kubwa kama kamba, mikeka, vikapu na magunia.

 “Tasnia ya mkonge iliporomoka kati ya mwaka 1984 hadi 2011 kutokana na ushindani wa bidhaa za plastiki. Hata hivyo, kwa sasa tasnia hii inapata uhai mpya kutokana na ongezeko la mahitaji ya bidhaa rafiki kwa mazingira, kama vifaa vya magari aina ya dashboardi,” amesema.

Katika hatua nyingine ya ubunifu, Kibasa ameeleza kuwa mabaki ya mkonge yanayotokana na usindikaji yanaweza kutumika kuzalisha uyoga, ambao una soko kubwa ndani na nje ya nchi, na hivyo kuongeza mapato kwa wakulima na wajasiriamali.

Ameongeza kuwa katika maonesho ya Nanenane mwaka huu, TSB inalenga kuwaelimisha wananchi kuhusu fursa zinazopatikana katika kilimo cha mkonge, ili kuchochea ushiriki wa Watanzania katika kuboresha maisha yao na kuchangia ustawi wa uchumi wa taifa.

Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), chini ya Wizara ya Kilimo, imeendelea kusimamia maendeleo ya zao hilo kwa kutoa elimu ya kilimo bora, teknolojia za kisasa za usindikaji, pamoja na kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi katika mnyororo mzima wa thamani wa mkonge.

Post a Comment

0 Comments

Mgomba wa Chama cha National League for Democracy (NLD),Doyo Hassan Doyo akiingia na usafiri wa bajaji  MC 816 CNUkuchukua fomu ya urais 2025.