KAPINGA AITAKA BRELA KUWAFIKIA WAFANYABIASHARA SABASABA

📍Wafanyabiashara Sabasaba kunufaika na huduma za BRELA

Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameielekeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA),kuwafuata wafanyabiashara wanaoshiriki Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) ili kuwapatia huduma za usajili na urasimishaji wa biashara moja kwa moja katika mabanda yao.

Akizungumza leo Julai 1, 2026, baada ya kutembelea mabanda ya BRELA yaliyopo ndani ya jengo la Wizara ya Viwanda na Biashara, Waziri Kapinga amesema BRELA inapaswa kuwa mshirika wa maendeleo kwa wafanyabiashara kwa kuwasaidia kutatua changamoto zinazowakabili badala ya kuwa chanzo cha hofu.

Amesisitiza kuwa maafisa wa BRELA wanapaswa kujipanga vizuri na kutembelea mabanda ya wafanyabiashara ili kuwahamasisha kurasimisha biashara zao na kuwapatia huduma kwa wakati, akieleza kuwa jukumu la taasisi hiyo ni kuwezesha biashara kukua na si kuwabana wafanyabiashara.

"Nendeni kama wawezeshaji wa biashara, si kama migambo. Wasaidieni wafanyabiashara kurasimisha biashara zao na kutatua changamoto zinazowakabili," amesema Waziri Kapinga.

Pia ameitaka BRELA kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi, wafanyabiashara na wadau wote wanaofika katika banda lake, ili kuhakikisha wanapata huduma kwa haraka, kwa urahisi na kwa ufanisi.

Miongoni mwa huduma zinazotolewa katika banda la BRELA ni usajili wa majina ya biashara, usajili wa kampuni, usajili wa alama za biashara na huduma, utoaji wa hataza, utoaji wa leseni za biashara Kundi A, leseni za viwanda pamoja na huduma mbalimbali zinazotolewa baada ya usajili.

Katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea tangu Juni 28, 2026, BRELA imeendelea kutoa huduma mbalimbali za papo kwa papo kupitia mfumo ulioboreshwa wa BRELA Online Services (BOS), hatua iliyowezesha wadau wengi kupata huduma kwa urahisi.

Post a Comment

0 Comments

TPDC YAELEZA MAFANIKIO YA UTAFITI WA MAFUTA NA GESI SABASABA