PPRA YAWATAKA VIJANA WENYE ULEMAVU KUNUFAIKA NA ZABUNI ZA SERIKALI


Na Asha Mwakyonde, RUKWA

UJUZI wa ufundi stadi unaweza kuwa daraja la vijana wenye ulemavu kuelekea kujitegemea kiuchumi iwapo wataunganishwa na fursa za masoko na zabuni za Serikali. Hayo yameelezwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), iliyowahimiza vijana hao kuunda vikundi na kujisajili katika Mfumo wa Kitaifa wa Ununuzi wa Kielektroniki Tanzania (NeST).

Wito huo umetolewa leo Oktoba 13,2026 na Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba,  alipotembelea banda la Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika Maonesho ya Wiki ya Vijana yanayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Sumbawanga, mkoani Rukwa.

Simba amesema vijana wenye ulemavu wanaohitimu mafunzo ya ufundi stadi wanapaswa kusaidiwa kutumia ujuzi wao kujipatia kipato na kujenga maisha ya kujitegemea, badala ya kuishia kupata vyeti bila kuunganishwa na fursa za kiuchumi.



Amesema kuanzisha vikundi na kujisajili katika mfumo wa NeST kutawawezesha vijana hao kushiriki katika zabuni za Serikali, kupata kazi na kukuza shughuli zao za uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma.

“Tunaiomba VETA kuongeza kasi ya kusajili makundi maalumu ili vijana hawa warasimishwe na kupata nafasi za kufanya kazi na Serikali,” amesema Simba.

Ameeleza kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma, taasisi za umma zinapaswa kutenga asilimia 30 ya bajeti zao za ununuzi kwa ajili ya makundi maalumu, yakiwemo vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.

Hata hivyo, amesema ili vijana wanufaike na fursa hizo, kuna umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya VETA, PPRA, benki na wadau wengine wa maendeleo ili kuwawezesha kupata vifaa vya kazi, utaalamu na masoko ya bidhaa na huduma wanazozalisha.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa watoa huduma waliopata zabuni kukamilisha kazi walizokabidhiwa kwa wakati na kulipwa stahiki zao kwa wakati, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuwajengea vijana imani na kuwahamasisha wengi zaidi kushiriki katika shughuli za kiuchumi.

Simba amebainisha kuwa uwezeshaji wa vijana haupaswi kuishia katika kuwapatia mafunzo ya ufundi stadi pekee, bali unapaswa kuendelea hadi kuwarasimisha, kuwaunganisha na masoko na kuwafungulia milango ya kushiriki katika zabuni za Serikali.

Amesema hatua hiyo itasaidia vijana wenye ulemavu kutumia ujuzi wao kujiajiri, kuongeza kipato na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Taifa.

Post a Comment

0 Comments

PPRA YANG'ARA KILELE MBIO ZA MWENGE WA UHURU 2026