Na Asha Mwakyonde, RUKWA
VIJANA wenye vipaji vya uchoraji na upakaji wa majengo wametakiwa kutumia fursa za mafunzo ya ufundi zinazotolewa na Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Kagera ili kukuza vipaji vyao na kujipatia ajira kupitia ujuzi wanaoupata.
Akizungumzia fursa hizo, leo Oktoba 12, 2026katika Maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayofanyika mkoani Rukwa, yenye kaulimbiu isemayo “Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo.” Samora Masebuka mwanafunzi wa 'Level ' ya tatu anayejihusisha na fani ya uchoraji na upakaji wa majengo ameeleza kuwa ujuzi katika fani hizo unaweza kuwasaidia vijana kujiajiri na kujenga maisha yao kupitia kazi za mikono.
Amesema fani ya uchoraji inahitaji kipaji, ambapo mafunzo yana umuhimu mkubwa katika kumwezesha mtu kuboresha uwezo wake na kufanya kazi kwa weledi.
Ameeleza kuwa alianza kujihusisha na uchoraji akiwa katika elimu ya sekondari, akitumia kipaji chake kuchora picha mbalimbali na kusaidia kazi za mapambo katika shughuli na maeneo tofauti.
Hata hivyo, amesema fursa za kupata kazi za uchoraji zilikuwa chache, jambo lililomfanya aendelee kutumia kipaji chake katika shughuli mbalimbali huku akijijengea uzoefu.
Amebainisha kuwa baadhi ya vijana wenye vipaji hukosa fursa ya kuviendeleza kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwamo kutokuelewa kwa baadhi ya wazazi umuhimu wa fani za ufundi.
Amesema mafunzo ya ufundi yanaweza kuwasaidia vijana kubadili vipaji vyao kuwa ujuzi unaoweza kuingiza kipato na kuwawezesha kujitegemea kiuchumi.
Kwa mujibu wa maelezo yake, mafunzo ya muda mfupi katika fani hizo yanagharimu takribani Sh 120,000 kwa wanakaa bweni huku mafunzo ya kila siku yakitajwa kugharimu Sh 60,000.
Ametoa wito kwa vijana wenye vipaji vya uchoraji, upakaji wa majengo na fani nyingine kutumia fursa zinazopatikana VETA Kagera na vyuo vingine vya ufundi nchini ili kupata ujuzi na kuongeza nafasi za kujiajiri.

0 Comments