SOS CHILDREN’S VILLAGES YAWAWEZESHA VIJANA KUJIAJIRI


Na Asha Mwakyonde, RUKWA

VIJANA wanaokabiliwa na changamoto za kifamilia na kijamii wanapata fursa ya kujenga maisha yao kupitia elimu ya ujasiriamali, mafunzo ya biashara na utengenezaji wa bidhaa zinazoweza kuwaingizia kipato, kupitia juhudi za Shirika lisilo la Kiserikali SOS Children’s Villages Tanzania.

Akizungumza leo Oktoba 12,2026 mkoani hapa katika Maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayofanyika mkoani Rukwa, yenye kaulimbiu isemayo “Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo.” Afisa Vijana kutoka Shirika hilo Philip Namanga, amesema shirika lina hakikisha kila mtoto anakuwa katika mazingira ya kifamilia yenye upendo, usalama, na usaidizi unaotakiwa ili kufikia uwezo wake kamili huku akisema 

watoto na vijana walio katika mazingira magumu, wakiwemo waliopoteza malezi ya familia na wale waliokatiza masomo kutokana na changamoto mbalimbali.

Namanga amesema shirika hilo linashirikiana na familia na wadau mbalimbali kuwasaidia vijana kupata ujuzi utakaowawezesha kujitegemea kiuchumi.

Amesema vijana wanaopata msaada huo hujengewa uwezo wa kuanzisha na kuendesha shughuli za biashara, kutengeneza bidhaa mbalimbali na kuzitangaza kwa wateja ili kupata kipato.

Ameeleza kuwa ushiriki wao katika maonesho hayo unalenga kuonesha uwezo wa vijana, bidhaa wanazotengeneza na hatua wanazopiga katika kujenga maisha yao kupitia ujasiriamali.

Namanga amebainisha kuwa ushirikiano na wadau mbalimbali umekuwa muhimu katika kuwasaidia vijana kujiamini, kutambua vipaji vyao na kutumia fursa zilizopo kujenga maisha bora.

"Shirika hili hushirikiana na idara za ustawi wa jamii katika kuwasaidia watoto wanaokabiliwa na changamoto za malezi, ikiwemo wale waliopoteza familia, waliopitia ukatili na wanaohitaji uangalizi maalumu," amesema.

Amesema pale inapowezekana na kuwa katika maslahi ya mtoto, juhudi hufanyika kushirikiana na familia zao ili kuboresha mazingira ya malezi na kuhakikisha watoto wanapata ulinzi na huduma zinazohitajika.


Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya familia, Serikali na taasisi zinazoshughulikia ustawi wa watoto ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama na kupata fursa za kujenga maisha yao ya baadaye.

Namanga ametoa wito kwa jamii kuendelea kushirikiana na taasisi zinazosaidia watoto na vijana walio katika mazingira magumu ili kuwajengea uwezo, kuimarisha malezi na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.

Post a Comment

0 Comments

VETA KAGERA YAWAFUNGULIA VIJANA FURSA ZA UCHORAJI NA UPAKAJI RANGI MAJENGO