Na Mwandishi Wetu, ANKARA – UTURUKI
TANZANIA na Uturuki zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika usimamizi wa maafa, ikiwemo matumizi ya teknolojia za kisasa, mafunzo ya wataalamu, utafutaji na uokoaji pamoja na mifumo ya ufuatiliaji na tahadhari za mapema.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, wakati wa kikao cha pamoja kati ya ujumbe wa Serikali ya Tanzania na uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Maafa na Dharura ya Uturuki (AFAD), kilichofanyika katika ofisi za taasisi hiyo mjini Ankara.
Kikao hicho ni sehemu ya ziara ya kikazi ya Dkt. Yonazi nchini Uturuki yenye lengo la kuongeza ujuzi na maarifa ya kiufundi, kuimarisha uwezo wa kitaasisi na kujifunza uzoefu wa nchi hiyo katika kupunguza vihatarishi vya maafa, kujiandaa na kukabiliana na dharura pamoja na kurejesha hali baada ya maafa.
Dkt. Yonazi amesema Tanzania inathamini uzoefu na utaalamu wa AFAD katika usimamizi jumuishi wa maafa na kwamba Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano huo kwa manufaa ya nchi hizo mbili.
Ameeleza kuwa maeneo yanayolengwa katika ushirikiano huo ni pamoja na kuendeleza mifumo ya kisasa ya usimamizi wa maafa, matumizi ya teknolojia, mafunzo ya wataalamu, utafutaji na uokoaji pamoja na uratibu wa hatua za mwitikio wakati wa dharura.
“Tanzania itaendelea kujifunza na kushirikiana na taasisi mbalimbali zenye uzoefu katika usimamizi wa maafa, ikiwemo AFAD, ili kuimarisha uwezo wa kitaifa wa kuzuia na kupunguza athari za maafa, kujiandaa, kukabiliana na kurejesha hali pindi yanapotokea,” amesema Dkt. Yonazi.
Kwa upande wake, Mkuu wa AFAD nchini humo, Gavana Ali Hamza Pehlivan, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendeleza ushirikiano na Uturuki katika eneo la usimamizi wa maafa na kusema taasisi hiyo iko tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali ya kitaalamu.
Gavana Pehlivan amesema maeneo hayo ni pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa katika usimamizi wa maafa, mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ya vihatarishi na madhara ya maafa, maandalizi na mwitikio wa dharura pamoja na uanzishaji, mafunzo na uendelevu wa timu maalumu za utafutaji na uokoaji.
Amefafanua kuwa AFAD inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia dhana ya usimamizi jumuishi wa maafa inayohusisha hatua zote za mzingo wa usimamizi wa maafa, kuanzia kutambua na kutathmini vihatarishi, kuzuia na kupunguza uwezekano na athari za maafa, kujiandaa na kukabiliana na dharura hadi kurejesha hali baada ya maafa.
Kwa mujibu wa Gavana Pehlivan, AFAD imejenga uwezo wa kuratibu timu za wataalamu na vikosi vya utafutaji na uokoaji vinavyoshughulikia majanga mbalimbali, yakiwemo matetemeko ya ardhi, mafuriko na dharura nyingine, kwa lengo la kuokoa maisha na kulinda mali.
Ameongeza kuwa taasisi hiyo pia hushiriki katika uratibu wa utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa waathirika wa maafa na kusaidia shughuli za kurejesha hali na makazi katika maeneo yaliyoathirika.
Katika eneo la kujenga uwezo wa rasilimali watu, AFAD inaendesha mafunzo na mazoezi ya vitendo kwa wataalamu na timu za mwitikio wa maafa kupitia miundombinu yake ya mafunzo, ikiwemo Disaster and Emergency Training Centre (AFADEM).
Amesema mafunzo hayo yanalenga kuongeza ujuzi wa kitaalamu, uwezo wa kufanya kazi kwa pamoja na utayari wa kukabiliana na matukio ya dharura.
Gavana Pehlivan pia amesema AFAD inashiriki katika ushirikiano wa kimataifa wa usimamizi wa maafa kupitia Timu ya Kimataifa ya Utafutaji na Uokoaji (INSARAG), inayoratibiwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (UN-OCHA), kwa kupeleka timu maalumu za utafutaji na uokoaji na kutoa msaada wa kibinadamu katika nchi mbalimbali pale yanapotokea maafa makubwa.
Tanzania na Uturuki zimeendelea kuwa na fursa ya kubadilishana uzoefu na utaalamu katika usimamizi wa maafa, hususan katika teknolojia, mifumo ya taarifa na tahadhari za mapema, mafunzo, utafutaji na uokoaji, uratibu wa mwitikio wa dharura na urejeshaji wa hali.
Ushirikiano huo unalenga kuimarisha uwezo wa taasisi na jamii katika kukabiliana na vihatarishi vya maafa na kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza pindi yanapotokea.







0 Comments