TUME YATOA MAELEKEZO KWA WATENDAJI WA UCHAGUZI


Na Mwandishi wetu,Tabora

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewataka watendaji wanaosimamia uchaguzi kutumia weledi, umakini na kujituma katika kutekeleza majukumu yao ili kuhakikisha uchaguzi mdogo wa Ubunge Jimbo la Chamwino na Udiwani katika kata 11 za Tanzania Bara unafanyika kwa ufanisi.

Wito huo umetolewa na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt. Zakia Mohammed Abubakar, mkoani Tabora jana, Oktoba 1, 2026, wakati akifunga mafunzo ya watendaji wa uchaguzi yaliyofanyika kwa siku tatu kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 1, 2026.

Dkt. Zakia anaeleza kuwa baada ya watendaji hao kupatiwa mafunzo, Tume inatarajia watatekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi, huku wakizingatia ratiba ya utekelezaji wa shughuli za uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Novemba 4, 2026.

“Ni matarajio ya Tume kwamba, baada ya kupatiwa mafunzo haya, mtatekeleza majukumu yenu kwa ufanisi na weledi mkizingatia ratiba ya utekelezaji ili kufanikisha uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Chamwino na Madiwani katika kata 11 za Tanzania Bara,” amesema.

Amewakumbusha watendaji hao kuwa shughuli zote za uchaguzi zinaongozwa na Katiba, sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi pamoja na maelekezo yanayotolewa na Tume.

Kwa msingi huo, amewataka kuendelea kutenga muda wa kusoma Katiba, sheria na maelekezo mbalimbali yatakayotolewa na Tume ili yawe mwongozo katika utekelezaji wa majukumu yao na usimamizi wa uchaguzi.

Aidha, Dkt. Zakia amesisitiza umuhimu wa kuzingatia sifa na uwezo wakati wa kuteua na kuajiri watendaji wa vituo vya kupigia kura, akieleza kuwa kundi hilo lina jukumu muhimu la kusimamia upigaji na uhesabuji wa kura vituoni.

“Kuhusu utaratibu wa kupata watendaji wa vituo, tunayo imani kuwa mtateua na kuajiri watendaji wenye sifa na uwezo wa kufanya kazi hii muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu,” amesema.

Ameongeza kuwa jambo hilo limekuwa likisisitizwa tangu siku ya kwanza ya mafunzo kwa sababu watendaji wa vituo ndio watakaokuwa mstari wa mbele kusimamia zoezi la kupiga na kuhesabu kura, kazi inayohitaji umahiri, umakini na weledi.

Dkt. Zakia pia amewataka watendaji kuhakikisha mafunzo kwa watendaji wa vituo vya kupigia kura yanafanyika kwa ufanisi na kuzingatia weledi, pamoja na ratiba iliyopangwa katika utekelezaji wa shughuli za uchaguzi.

Mafunzo hayo yamewahusisha Waratibu wa Uchaguzi wa Mikoa, Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi Ngazi ya Jimbo, Wasimamizi wa Uchaguzi Ngazi ya Kata, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ununuzi na Wahasibu.

Uchaguzi wa Udiwani utafanyika katika kata 11 za Tanzania Bara ambazo ni Nonde, Halmashauri ya Jiji la Mbeya; Lugenge, Halmashauri ya Mji Njombe; Bargish, Halmashauri ya Mji Mbulu; Makole, Halmashauri ya Wilaya ya Muheza; Mwera, Halmashauri ya Wilaya ya Pangani na Oldonyosambu, Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.

Kata nyingine ni Igalula, Halmashauri ya Wilaya ya Uyui; Shelui, Halmashauri ya Wilaya ya Iramba; Mvumi, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa; Nyarero, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Ilolangulu, Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe.

Post a Comment

0 Comments

USAFI WA MIFEREJI, KARAVATI NA MADARAJA :NGUZO YA KUIMARISHA BARABARAKATIKA MSIMU WA MVUA