WAZEE WAFURAHISHWA NA MIUNDOMBINU JIJINI DODOMA


Na WMJJWM, DODOMA

VIONGOZI na wawakilishi wa Baraza la Ushauri la Wazee Taifa wameeleza kufurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa miundombinu jijini Dodoma, wakisema uwepo wake unarahisisha utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi.

Wazee hao wameeleza hayo Oktoba 2, 2026, baada ya kufanya ziara iliyoratibiwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, kwa lengo la kuwawezesha kujifunza na kujionea maendeleo ya miundombinu pamoja na vivutio mbalimbali vinavyopatikana jijini Dodoma.

Ziara hiyo imefanyika ikiwa sehemu ya shughuli za kuadhimisha Siku ya Wazee Duniani, inayoadhimishwa Oktoba Mosi kila mwaka, huku kwa mwaka huu kilele cha maadhimisho hayo kikitarajiwa kufanyika Novemba 4, mkoani Songwe.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Taifa, David Sendo, amesema Serikali imeendelea kufanya kazi kubwa katika ujenzi wa miundombinu, hatua ambayo imechangia kurahisisha upatikanaji na utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Tunampongeza Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya katika ujenzi wa miundombinu. Tumejionea Kituo cha Treni ya Kisasa cha Samia jijini Dodoma, ni kizuri sana na tunafurahishwa na hilo,” amesema Sendo.

Ameongeza kuwa wazee wanatoa wito kwa jamii kutunza miundombinu hiyo na kuitumia kwa usahihi ili iweze kudumu na kuendelea kuwa na manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Katika ziara hiyo, wazee hao walitembelea maeneo mbalimbali jijini Dodoma, ikiwemo Uwanja wa Ndege, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Mji wa Serikali Mtumba na Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Ziara hiyo imewapa fursa wazee hao kujionea kwa karibu maendeleo ya miundombinu na huduma zinazotolewa katika maeneo hayo, ikiwa ni sehemu ya kuongeza uelewa wao kuhusu maendeleo yanayofanyika nchini.



Post a Comment

0 Comments

USAFI WA MIFEREJI, KARAVATI NA MADARAJA :NGUZO YA KUIMARISHA BARABARAKATIKA MSIMU WA MVUA