SEQUIP YAMVUSHA NEEMA KUTOKA KIDATO CHA PILI HADI CHUO KIKUU


 Na Mwandishi Wetu

CHANGAMOTO za maisha, ikiwemo ujauzito, umaskini na kupoteza mzazi, hazikuwa mwisho wa safari ya elimu kwa Neema Andrea Usia, ambaye baada ya kukatisha masomo akiwa kidato cha pili ameweza kurejea shuleni kupitia Mradi wa SEQUIP na hatimaye kujiunga na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).

Safari ya Neema ni ushuhuda wa namna fursa ya pili ya elimu inavyoweza kubadili maisha ya msichana na kumrejeshea matumaini ya kutimiza ndoto zake ambazo hapo awali zilionekana kufifia kutokana na mazingira magumu ya maisha.

Akielezea safari yake ya elimu, Neema anasema alimaliza elimu ya msingi mwaka 2013 kwa daraja B na kuchaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Luiwa, Wilaya ya Mbalali, lakini alilazimika kuacha masomo akiwa kidato cha pili kutokana na changamoto za kiuchumi katika familia, kifo cha mama yake na kupata ujauzito.

Anasema baada ya kukatisha masomo alirejea nyumbani, ambako alikabiliwa na jukumu la kumlea mtoto bila msaada wa baba wa mtoto, hali iliyomfanya aanze kujitafutia kipato kwa kuanzisha biashara ndogo ya genge ili kukidhi mahitaji yake na mtoto.

Hata hivyo, ndoto ya kuendelea na elimu haikufutika. Mwaka 2022 alipata taarifa kutoka kwa mwalimu wake wa zamani kuhusu mpango wa Serikali wa kuwapa nafasi nyingine wasichana waliokatisha masomo kurejea katika mfumo wa elimu.

Taarifa hiyo ilimpa matumaini mapya na kumshawishi kutumia fursa hiyo kuanza upya safari yake ya masomo kupitia Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP).

Neema alijiunga na kituo cha masomo katika Shule ya Sekondari Iyai, Wilaya ya Mbalali, kabla ya kuhamishiwa Shule ya Sekondari Kiwira, Wilaya ya Rungwe, baada ya kituo cha awali kufungwa.

Akiwa Kiwira, alisoma hatua ya kwanza na kufanya mtihani wa Maarifa ya Elimu ya Sekondari (QT), ambapo alifaulu na kuendelea na masomo ya kidato cha tatu na cha nne.

Juhudi zake zilizaa matunda baada ya kufanya mtihani wa kidato cha nne katika Kituo cha Rubala na kupata Division II, matokeo yaliyomuwezesha kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Mwakaleli.

Awali alichaguliwa tahasusi ya HGL, lakini kutokana na shauku yake ya kusoma masomo ya sayansi, alibadilisha na kujiunga na tahasusi ya CBG.

Neema anasema ushirikiano alioupata kutoka kwa walimu na uongozi wa shule ulimsaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali na kuendelea kupambana katika masomo yake hadi alipofanya mtihani wa kidato cha sita na kupata Division I ya pointi nane.

Matokeo hayo yalimfungulia milango ya elimu ya juu baada ya kuchaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), ambako anasomea Shahada ya Sayansi katika Sayansi na Teknolojia ya Chakula (Bachelor of Science in Food Science and Technology).

Akizungumzia mafanikio hayo, Neema anaeleza kuwa fursa ya kurejea shuleni imekuwa mabadiliko makubwa katika maisha yake, akitoa shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira yanayowawezesha wasichana waliokatisha masomo kupata nafasi nyingine ya kuendelea na elimu.

Anasisitiza kuwa wasichana wengi waliokumbana na changamoto zinazofanana na zake bado wana ndoto za kielimu, hivyo wanahitaji kupewa fursa na kuhamasishwa kuitumia ili waweze kujenga maisha bora na kufikia malengo yao.

Safari ya Neema, kutoka kukatisha masomo akiwa kidato cha pili hadi kuanza masomo ya chuo kikuu, inaonesha umuhimu wa kuwapa wasichana waliokatisha masomo nafasi ya pili ya elimu, huku Mradi wa SEQUIP ukiendelea kuwawezesha kurejea katika mfumo wa elimu na kujenga upya matumaini ya maisha yao.

Post a Comment

0 Comments

ZAIDI YA SH. MILIONI 600 ZATUMIKA KUWEKEZA KATIKA MIUNDOMBINU YA KITUO CHA TAASISI YA ELIMU YA WATU WAZIMA IRINGA