MKUMBO ARIDHISHWA NA MAANDALIZI YA UZINDUZI MTUMBA


Na Asha Mwakyonde, DODOMA

MAANDALIZI ya uzinduzi wa majengo ya ofisi za Wizara na Taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma yamekamilika kwa hatua inayoridhisha, huku Serikali ikiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo linalotarajiwa kufanyika kesho, Oktoba 30, 2026.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, ameeleza kuridhishwa na maandalizi hayo baada ya kukagua maeneo mbalimbali yatakayotumika katika hafla ya uzinduzi huo, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi.

Katika ziara hiyo iliyofanyika Oktoba 29, 2026, Prof. Mkumbo alikagua geti kuu la kuingilia Mji wa Serikali Mtumba, maeneo ya uwekaji mawe ya msingi kwa ajili ya uzinduzi wa majengo ya Serikali na barabara za lami, pamoja na Uwanja wa Mashujaa utakaotumika kufanyika kwa hafla hiyo.

Baada ya ukaguzi huo, Prof. Mkumbo alipongeza hatua iliyofikiwa katika maandalizi na kutoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia uzinduzi huo, alioutaja kuwa tukio la kihistoria kwa Taifa.

Uzinduzi huo unatarajiwa kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiambatana na mgeni maalumu, Rais wa Jamhuri ya Angola, João Manuel Gonçalves Lourenço.

Hafla hiyo inalenga kuzindua majengo ya ofisi za Wizara na Taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami zilizojengwa katika Mji wa Serikali Mtumba, ambao ni eneo muhimu katika shughuli za kiutawala za Serikali jijini Dodoma.

Katika ziara hiyo, Prof. Mkumbo aliambatana na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi; Naibu Katibu Mkuu wa ofisi hiyo, Dkt. James Kilabuko; Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali, Paul Sangawe, pamoja na maafisa wengine wa Serikali.

Post a Comment

0 Comments

RC SENYAMULE : UPIGAJI WA FATAKI NI ISHARA YA HISTORIA KUBWA MTUMBA - DODOMA