MAMA NA BABA LISHE WATAKA FURSA ZA BIASHARA MTUMBA


 Na Asha Mwakyonde, DODOMA

WAFANYABIASHARA wadogo wanaweza kuwa miongoni mwa wanufaika wa uwekezaji wa Serikali katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, iwapo watatengwa maeneo maalumu ya kuendesha biashara zao. Hayo yameelezwa na Umoja wa Mama na Baba Lishe Tanzania, ambao umeiomba Serikali kuwatengea maeneo ya kuandaa na kuuza chakula kwa watumishi wa umma na wageni wanaofika katika mji huo.

Ombi hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Mama na Baba Lishe Tanzania, Viwaja Omali, wakati wa ziara ya kutembelea majengo na miundombinu ya Mji wa Serikali Mtumba, ambapo amepongeza uwekezaji uliofanywa na Serikali katika ujenzi wa majengo ya kisasa na barabara za lami.

Omali amesema wamevutiwa na muonekano wa mji huo pamoja na ukubwa wa majengo ya ofisi, akieleza kuwa maendeleo hayo yanatoa fursa za kiuchumi ambazo wafanyabiashara wadogo wanapaswa kuzipata.

“Tunaiomba Serikali, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, itutengee eneo maalumu la mama na baba lishe katika Mji wa Serikali Mtumba ili nasi tuweze kupata fursa ya kuuza chakula kwa watumishi wa Serikali na wageni wanaofika hapa,” amesema.

Ameeleza kuwa kutengwa kwa maeneo hayo kutawawezesha wafanyabiashara hao kuongeza kipato, kupanua shughuli zao na kunufaika na mzunguko wa kiuchumi unaoweza kuchochewa na uwepo wa watumishi wa umma na wageni katika mji huo.

Aidha, Omali ameiomba Wizara ya Maji kuhakikisha maeneo yatakayotengwa kwa ajili ya biashara hizo yanapatiwa huduma ya maji ya uhakika ili kurahisisha maandalizi ya chakula, usafishaji wa vyombo na unawaji wa mikono kwa wateja.

Amesema upatikanaji wa maji ya kutosha utasaidia kupunguza gharama za kununua maji kwenye madumu, huku ukiboresha usafi wa mazingira ya biashara na usalama wa chakula kinachouzwa.

Kwa upande wake, Katibu wa Umoja wa Mama na Baba Lishe Tanzania (UMALITA), Juliet Madacha, amesema ziara hiyo imelenga kutembelea taasisi na wizara zinazohusiana moja kwa moja na shughuli za wafanyabiashara hao.

Madacha amezitaja Wizara za Maji, Nishati, Afya, Maendeleo ya Jamii pamoja na Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuwa miongoni mwa taasisi muhimu wanazokusudia kuzitembelea kutokana na uhusiano wake na shughuli za mama na baba lishe.

Amefafanua kuwa Wizara ya Nishati ni muhimu katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, akibainisha kuwa umoja huo unalenga kuongeza matumizi ya nishati hiyo miongoni mwa wanachama wake.

Amesisitiza kuwa ziara hizo ni sehemu ya jitihada za kujenga uhusiano na taasisi za Serikali na kutafuta fursa zinazoweza kuboresha mazingira ya kazi na maendeleo ya kiuchumi ya mama na baba lishe nchini.

Post a Comment

0 Comments

RC SENYAMULE : UPIGAJI WA FATAKI NI ISHARA YA HISTORIA KUBWA MTUMBA - DODOMA