Wanafunzi wakipata maelezo kuhusu madhara ya dawa za kulevya walipotembelea banda la Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamabana na Dawa za Kulevya (DCEA).
NA ASHA MWAKYONDE, MBEYA
KAMISHNA wa Kinga na Tiba wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamabana na Dawa za Kulevya (DCEA),Dkt. Peter Mfisi, amewaasa wakulima kutojuhusisha na kilimo cha mirungi na bangi kwa kuwa mazao hayo ni haramu na yanadhibitiwa kisheria na badala yake walime mazao mengine ya chakulanl na biashara yakiwamo mahindi.
Akizungumza jijini Mbeya Agosti 5,2022 katika maonesho ya wakulima na wafugaji maarufu nane nane yanayoendelea kwenye viwanja vya John Mwakangale ambapo kitaifa yanafanyika mkoani hapa amesema adhabu ya kukutwa na kosa la kulima mazao haramu ni kifungo cha miaka 30 au kwenda jela kifungo cha maisha.
Dk. Mfisi ameeleza kuwa mkulima akilima bangi au mirungi uhakika wa kuvuna ni mdogo mkulima huyo anaweza akavuna na akihifadhi nyumbani kwake mamlaka itamfikia na kumkamata.
"Mkulima wa bangi au mirungi akikamatwa Ardhi yake itachukuliwa kuna vifungo virefu miaka 30 au kwenda jela kifungo cha maisha, hivyo tunawaomba wananchi waje kwenye maonesho haya kupata elimu," amesema Dk. Mfisi.
Dk. Mfisi ameongeza kuwa mbali elimu hiyo wananchi hao wafike katika banda hilo ili kujionea aina za dawa za kulevya wasije wakadanganywa wakambiwa ni pipi na kama kuna mtu anauza waende kuripoti katika mamlaka hiyo.
Kamishina huyo amefafanua kuwa mamlaka ya Kudhibiti na Kupamabana na Dawa za Kulevya ni taasisi ya serikali iliyopo chini ya ofisi ya Waziri Mkuu ilianzishwa mwaka 2017 kwa lengo la kuimarisha vita dhidi ya dawa za kulevya.
Amesema mamlaka hiyo inafanya kazi zake kwa kufuata mikakati mikuu minee ambayo ni kuhakikisha inapunguza uingizaji, uzalishaji na usambazaji wa dawa za kulevya nchini.
Dk.Mfisi amesema kuwa mikakati miongine ni kuhakikisha inatoa elimu kwa jamii ili ielewe madhara yatokanayo na dawa za kulevya, kupunguza madhara yalitokana na dawa hizo na mkakati wa nne ni kuimarisha ushirikiano wa Kanda na Taifa.
"Dawa za kulevya ni biashara inayovuka mipaka na wauzaji wa dawa hizi hawana mikapa wanaweza wakawa wanaishi Dar es Salaam lakini wanavuka mipaka," amesema Dk. Mfisi.
0 Comments