LATRA: WATAKAOKAIDI MFUMO WA KIELEKTRONIKI TUTAWACHUKULIA HATUA


NA ASHA MWAKYONDE, MBEYA

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imesema itawachukulia hatua kali wamililiki wa mabasi watakaokaidi kuingiza mabasi kwenye mfumo wa ukataji tiketi kwa njia ya mtandao ifikapo Agosti 30 mwaka huu.

Aidha Mamlaka hiyo imesema hadi kufikia jana tiketi zilizouzwa kwa njia ya mtandao E Tiketi zilikuwa 9,728.

Akizungumza katika maonyesho ya kitaifa ya Nane Nane yanayoendelea katika viwanja vya John Mwakangale Mkurugenzi wa Usalama Barabarani Johansen Kahatano amesema moja ya hatua ambazo zitachukuliwa dhidi yao ni pamoja na mabasi kufungiwa,kupigwa faini pamoja na kushusha abiria kama watakutwa barabarani wamepakia ili hali hawapo kwenye mfumo huo.

Kutokana na hilo ametoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri barabarani wanapaswa kusajili mabasi yao kwenye mfumo kabla ya tarehe ya mwisho ya kusajili iliotangazwa.

"Nawaomba wamiliki wa mabasi kusajili mabasi yenu katika mfumo,mahitaji kuona kila basi lipo kwenye mfumo ili kuepuka kufungiwa,"amesema Kahatano.

Amesema wenye mabasi wakifanya hivyo itasaidia kujua usalama wa magari barabarani ikiwemo kuona kama yanakwenda kinyume na mwendo uliopangwa yanapokuwa katika ruti zao za kila siku.

Hata hivyo amesema idadi ya mabasi iliopo nchi nzima ni 7,500 lakini yanayofanya kazi kila siku ni machache,na kutolea mfano mabasi yaliyotoka leo kwenye mfumo ni 4,500.

Akizungumzia mfumo wa E tiketi amesema hadi jana tiketi zilizouzwa kwa mtandao ni 9,728 huku akisisitiza jamii idai E tiketi pale inapofika kwenye ofisi kwa ajili ya kukata tiketi ya safari.

"Naomba jamii ijenge utaratibu wa kuomba E tiketi pale wanapokuwa wanauhitaji wa tiketi za safari,"amesema Kahatano.


Post a Comment

0 Comments

DKT. BITEKO ASISITIZA UMUHIMU WA MIFUMO THABITI YA NISHATI JADIDIFU KUKIDHI MAHITAJI YA NISHATI