WAZIRI NDAKI KUWA MGENI RASMI MAADHIMISHO YA WIKI YA KICHAA CHA MBWA

NA ASHA MWAKYONDE, DODOMA

SERIKALI kupitia Wizara ya Mifungo na Uvuvi imesema katika maadhimisho ya wiki ya kichaa cha Mbwa Duniani inatarajia kuchanja mbwa na paka 60,000, ikiwa ni kilele cha maadhimisho hayo ambayo kitaifa yatafanyika jijini hapa Septemba 28, mwaka huu na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Mifugo Mashimba Ndaki,yenye Kauli Mbinu isemayo Kichaa cha mbwa, Afya moja, Vifo sifuri (Rabies, One health, Zero deaths).

Pia imewataka wananchi kuendelea kufuatilia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ili kupata elimu  inayohusiana na masula ya ufugaji mbwa na paka lengo likiwa ni kuepuka madhara ya kung’atwa na mbwa.

Akizungumza jijini hapa leo Septemba 24, 2O22,Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, kutoka Wizara hiyo Profesa Hezron Nonga,amesema kuwa katika maadhimisho hayo watatoa chanjo bure maeneo tofauti tofauti nchini.

Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa maadhimisho hayo pia yatafanyika katika kanda nane huku akizitaja baadhi ya kanda hizo kuwa ni Temeke jijini Dar es Salaam,Arusha, Iringa, Mwanza, Tabora na Mtwara hivyo  huduma za chanjo zitatolewa bure kwa mbwa na paka.

Ameeleza kwamba maadhimisho hayo yatafanyika katika vituo vyote vya huduma za mifugo nchini, na kutakuwa na huduma ya kuchanja bure mbwa na paka ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wananchi kuhusu ufugaji bora wa mbwa.

“Tuna maafisa mifugo nchi nzima kila wilaya katika halmashauri 184 wao watakuwa wanatoa chanjo hizi, hivyo karibu robo tatu ya Watanzania watafikiwa na elimu hii ya huduma za kinga zinazoendana na taadhari ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa,” ameeleza.

Ameongeza kuwa kichaa cha mbwa kinaua, hivyo amewataka wananchi kuzuia kwa kuchanja mbwa na paka wao kila mwaka ili kuilinda za  jamii.

“Epuka kuwa katika mazingira ya kung’atwa na mbwa na endapo umengatwa, osha jeraha kwa sabuni na maji mengi yanayotiririka kwa dakika 15 na kidonda kisifungwe, kisha nenda haraka kwenye kituo cha kutolea huduma za afya,”amesema.

Akitoa mwenendo wa chanjo dhidi ya kichaa cha mbwa Prof, Nonga amesema mwaka 2020/2021 walichanja mbwa dozi 986,195 na paka 5,152 na 2021/2022, 1,608,344 pamoja na paka 6,833 na mwaka wa fedha 2022/2023 kuanzia Julai hadi Septemba wamechanja mbwa 323,638 na paka 28,933 kwenye halmashauri 101 ambapo katika madhimisho hayo wizara hiyo inatarajia kuchanja mbwa na paka 60,000.

Kichaa cha mbwa ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vya kichaa cha mbwa na huathiri wanyama wote hususan mbwa na binadamu na hauna tiba bali unakingwa kwa chanjo na kuzingatia ufugaji bora wa mbwa.

Pia kichaa cha mbwa huambiza kwa njia ya kung’atwa na mbwa mwenye ugonjwa huo na binadamu pia anaweza kuambukizwa kwa kugusa mate ya mbwa mwenye kichaa.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI