WAKURUGENZI WA HALMASHAURI WAMETAKIWA KUTOA ELIMU YA UPANGAJI WA MATUMIZI YA ARDHI KWA WANANCHI

 

Na Asha Mwakyonde, Dodoma

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete ametoa rai kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kutoa kipaumbele kuhusu utoaji elimu ya upangaji wa matumizi ya ardhi na kuhimiza uandaaji na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika miji, miji midogo na vijiji. 

Pia amekiri kuwapo na changamoto ya uhaba wa Wataalam wa Mipangomiji katika Bodi hiyo na nchini kwa ujumla na kwamba ili kukabiliana na changamoto hiyo Bodi kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, itaendelea kuomba vibali vya uhamisho wa watumishi kuhamia Bodi, kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na kuwajengea uwezo watumishi waliopo.

Rai hiyo ameitoa leo Januari 26,2023 wakati akizindua Bodi ya mpya ya Wakurugenzi ya Usajili wa Watalaam wa Mipango Miji,amesema kuwa uzinduzi wa Bodi hii ni suala muhimu sana katika mustakabali wa ukuaji wa taaluma ya Mipangomiji, kwani Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Menejimenti ya Bodi ndizo pande mbili ambazo zinaungana pamoja katika kuikuza na kuisimamia taaluma ya mipangomiji nchini. 

Naibu Waziri huyo amesema Suala la kupanga ardhi kwa nchi nzima, mijini na vijijini linatokana na ukweli kwamba rasilimali ardhi haiongezeki wakati idadi ya watu na shughuli zao zinaongezeka huku akitolea mfano Tanzania ina eneo lenye ukubwa wa takribani kilometa za mraba 948,132.89, ikijumuisha kilometa za mraba 62,032.89 za maji. Eneo la nchi kavu lina ukubwa wa kilometa za mraba 886,100, ambapo Tanzania bara ni kilometa za mraba 883,600, na Zanzibar ni kilometa za mraba 2,500.

Amesema kumekuwa na ongezeko la watu kutoka watu 43,625,354 (Sensa ya watu 2012) hadi kufikia watu 61,741,120 (Sensa ya Watu na Makazi 2022) na wakati idadi ya watu ikiongezeka, ukubwa wa ardhi bado ni uleule. 

"Kwa kuzingatia ukweli huo, Wataalam wetu pamoja na kampuni za upangaji miji ni muhimu ziendelee kupanga ardhi kwa weledi wa hali ya juu kwani ikifanyika vinginevyo, tutashuhudia ongezeko la migogoro ya ardhi baina ya watumiaji mbalimbali wakiwemo wakulima, wafugaji, wachimbaji madini na hifadhi za Taifa," amesema.


Ameeleza kuwa sekta ya Ardhi ni muhimu kwa maendeleo y Taifa na kwa kila mwananchi na ni msingi wa kipekee wa maendeleo na ni rasilimali isiyoongezeka. 

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu WA wizara hiyo Seushi Mburi amesema kuwa Wizara ya Ardhi itaendelea kushirikiana na Bodi mpya katika kutekeleza majukumu yake.

"Kukiwa na migogoro mingi inatokana na kukosa Mipango miji mizuri, hivyo wizara ipo tayari kushirikiana na Bodi hii," ameeleza Kaimu Katibu Mkuu huyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi hiyo Prof.John Lupala amesema bodi hiyo itafanya kazi ya kusimamia utekelezaji wa bodi kwa kuzingatia sheria na kanuni zinazoongoza mipango Miji. 

Amesema kwa kuzingatia uzoefu na weledi walionao katika fani mbalimbali watashirikiana kikamilifu na Wizara kuendeleza taaluma ya Mipangomiji kwa pamoja na kufikia lengo la kusimamia Wataalam wa Mipangomiji na kampuni za upangaji miji. 

Prof.Lupala amesema bodi hiyo itasimamia Wataalam na Kampuni za Mipangomiji kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu za upangaji miji, kutoa huduma bora, kuweka mazingira ya kuvutia Wataalam wa Mipangomji waliokidhi vigezo vya kusajiliwa ili wasajiliwe, pia kuzalisha fursa zaidi za ajira na kuongeza mchango katika pato la taifa.

Amesema kwa mujibu wa Sheria, Bodi imepewa dhamana ya kuisimamia taaluma ya Mipangomiji pamoja na Wataalam wa Mipangomiji, hivyo watahakikisha wanaweka mipango kuifanya taaluma ijulikane kwa wananchi na pale ambapo mtaalam au kampuni imefanya kazi kinyume na maadili zichukuliwe hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria.  
 
"Tunaahidi kufanya kazi kwa uadilifu na weledi wa hali ya juu, kwa maslahi mapana ya nchi yetu na kwa kuzingatia Sheria na Kanuni zilizopo ili kuhakikisha kwamba, Bodi inakidhi matarajio ya wadau na kuleta tija katika utekelezaji wa majukumu lakini jambo kubwa zaidi tutabuni mbinu za namna bora ya kuimarisha utendaji kazi wa Wataalam na Kampuni za Upangaji Miji pamoja na kuibua mikakati ya kutatua changamoto zinazoikabili taaluma hii na Sekta ya Ardhi kwa ujumla,"amesisitiza  
 
Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri amesema kuwa ili ardhi ithaminiwe lazima kuwe na uhifadhi ardhi ili miji ipangwe na kuwa na hadhi nzuri.

Aidha ameishauri bodi hiyo kutengeneza na kuandaa mpango kazi wa ardhi ili kuboresha miundombinu ya majiji 
ikiwa ni pamoja na kusajili wataalamu wa ardhi kwa kuhusisha makampuni ya upimaji ardhi kuondoa migogoro ya ardhi.

Mkuu huyo wa Wilaya pia ameishauri elimu kwa Umma ifanyike ili wananchi wajue namna ya kuimiliki ardhi kihalali na kuondokana na migogoro iliyopo ambayo kwa kiasi fulani inakwamisha shughuli za maendeleo.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU