BONANZA LA WABUNGE KUFANYIKA JANUARI 28, MWAKA HUU DODOMA


 Na Asha Mwakyonde, Dodoma

SPIKA wa Bunge la Tanzania Dk. Tulia Ackson amesema kuwa Ofisi ya Bunge hilo imeanzisha utaratibu wa bonanza la michezo lenye lengo la kutoa fursa ya kukutanisha wabunge,watumishi Pamoja na wadau mbalimbali katika mazingira rafiki nje ya Bunge.

Kauli mbiu ya Bonanza hilo ni "Bunge Bonanza: Shiriki Michezo, Jenga Taifa lenye Afya".ambalo litawapunguzia wabunge na wadua hatari ya kupata maradhi sugu yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari, shinikizo la damu,uzito uliopitiliza, kuimarisha mifupa na miauli, kuongeza Uhimili (stamina), utimamu wa mwili (Body fitness),kuondoa dalili za msongo wa mawazo, kuimarisha afya ya akili na kuongeza uwezo wa kufikiri na hatimaye kuwa na afya njema.

Akizungumza Jijini Dodoma leo Januari 26,2023, Dk. Tulia amesema bonanza hilo litakuwa linafanyika mara nne kila mwaka ambapo kutakuwa na mambonanza madogo (Pre-Bonanza), matatu wakati wa mikutano mifupi ya Bunge na moja kubwa (Grand Bonanza), wakati mkutano wa bajeti.

Dk. Tulia Amefafanua kuwa lengo ni kufahamiana zaidi na kujenga umoja utakaosaidia katika utekelezaji wa majukumu yao.

"Bonanza la kwanza litafanyika siku ya jumamosi Januari 28,2023 katika viwanja vya shule ya sekondari ya John Merlin, litaanza na matembezi yatakayoanzia Chuo cha Mipango Dodoma na kuishia shule ya sekondari ya John Merlin," ameeleza.

Amesema bonanza hilo litahusisha michezo mbalimbali ambayo ni mpira wa miguu, kikapu,Pete , wavu wa meza, pool table,kurusha vishale,riadha na kutembea kwa haraka.

Dk. Tulia ameongeza kuwa baada ya Bonanza hilo kumalizika matarajio yake ni kuona wabunge na watumishi watajiwekea utaratibu wa kufanya mazoezi mara kwa mara.

"Kuanzishwa kwa bonanza hili hakufuti ushiriki wetu katika michezo mingine ya kirafiki na michezo inayotukutanisha na wanamichezo wengine kutoka mabunge ikiwa ni pamoja na michezo ya mabunge ya Jumuiya ya Afrika mashariki (EALA)," amesema.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI