DK.KIMAMBO: ASILIMIA 40 YA WATOTO WA SHULE WANA TATIZO LA KUTOBOKA MENO


Na Asha Mwakyonde DODOMA 

UTAFITI umeonyesha kuwa takriban asilimia 40 ya watoto wa shule nchini wanakutana na matatizo ya kutoboka kwa meno (Dental Caries), huku sababu kubwa ikielezwa ni kutokana na tabia za kula vyakula vyenye sukari nyingi kama pipi, soda, na vyakula vya haraka, bila kutunza usafi wa kinywa. 

Akizungumzia tatizo la kutoboka kwa meno, katika mahojiano maalum,Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Kinywa na Meno kutoka Hospitali Rufaa ya Kanda ya Kati ya Benjamin Mkapa (BMH),Dk.Alex Kimambo amesema tatizo ni kubwa hapa nchini ambapo linaathiri hasa watoto na vijana.

Daktari huyo amesema hali hiyo inazidi kuwa mbaya kwa watoto, ambao mara nyingi hapigi mswaki meno vyao vizuri au mara kwa mara.

Akizungumzia suala la elimu ameeleza upungufu wa elimu kuhusu Afya ya Kinywa na meno bado haijafika kwa undani katika maeneo mengi nchini, hasa vijijini.

"Watu wengi hawajui jinsi ya kutunza afya ya kinywa na meno, kama vile umuhimu wa kupiga mswaki mara mbili kwa siku, kula vyakula bora, na kutembelea daktari wa meno mara kwa mara," ameeleza.

Ameongeza kuwa uwepo wa huduma za afya ya kinywa katika baadhi ya maeneo ni mdogo, na hivyo watu wengi hawawezi kupata huduma bora za meno.

Daktari huyo amesema huduma za afya ya meno ingawa zinapatikana katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mwanza , huduma hizo bado ni chache na kwamba hazipatikani kwa urahisi haswa katika maeneo ya vijijini na maeneo ya pembezoni. 

"Hali hii hufanya watu wengi kukosa huduma za uchunguzi na matibabu ya meno," ameeleza Dk.Kimambo.

Amsema udaktari wa kinywa na meno ni taaluma inayohitajika nchini na kwamba kuna uhaba wa wataalamu hao, hasa katika maeneo ya vijijini.

Dk.Kimambo amesema hiyo ni changamoto kubwa kwa kuhakikisha kuwa watu wanapata huduma bora.

Akizungumzia juhudi za Serikali na Mashirika amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya, imekuwa ikifanya juhudi za kuongeza ufanisi katika huduma za afya ya kinywa na meno hiyo ni pamoja na kuanzisha kampeni za kuhamasisha usafi wa kinywa, kutoa huduma za bure au za gharama nafuu kwenye vituo vya afya.

Dk.Kimambo ameongeza kuwa juhudi nyingine zilizofanywa na serikali ni kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kutunza afya ya kinywa na kwamba miaka ya hivi karibuni usambazaji wa vifaa tiba vya kinywa na meno hadi ngazi za Halmashauri karibu zote nchini zilipata vifaa hivyo.

Aidha amesema kuwa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), yanafanya kazi ya kutoa elimu na huduma za afya ya meno kwa jamii, hasa katika maeneo ya vijijini.

Post a Comment

0 Comments

WAUGUZI, WAKUNGA ENDELENI KUBEBA DHAMANA KAMA SERIKALI ILIVYOWEKEZA