Na Asha Mwakyonde,Dodoma
SEKTA ya Ardhi ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa na kwa kila mwananchi pia ni msingi wa kipekee wa maendeleo na ni rasilimali isiyoongezeka.
Tanzania ina eneo lenye ukubwa wa takribani kilometa za mraba 948,132.89, ikijumuisha kilometa za mraba 62,032.89 za maji na Eneo la nchi kavu lina ukubwa wa kilometa za mraba 886,100, ambapo Tanzania bara ni kilometa za mraba 883,600, na Zanzibar ni kilometa za mraba 2,500.
Kumekuwa na ongezeko la watu kutoka watu 43,625,354 Sensa ya watu 2012 hadi kufikia watu 61,741,120 Sensa ya Watu na Makazi 2022.
Ni ukweli usiopingika ardhi ina faida kwa watumiaji wa sekta zote wakiwemo wakulima, wafugaji, wachimbaji madini na hifadhi za Taifa.
Asilimia 61 ya Watanzania wote wapo kwenye sekta ya kilimo ambayo inachangia asilimia 26 tu ya pato la Taifa.
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inahakikisha inawainua wakulima na kukiinua kilimo cha Tanzania ili kufikia lengo la kukuza sekta ya Kilimo kwa asilimia 10 ambayo imepewa jina la Agenda ya 10/30.
Wakulima,wawekezaji wanazungimzia ardhi inavyowabufaisha kupitia kilimo ikiwa ni pamoja na kupata mazao ya chakula na ya biashara.
Kupitia ardhi ili waweze kunufaika zaidi katika uwekezaji wao wanatumia mbinu nyingi zikiwamo kuweka mbolea, kupulizia dawa za kuzui wadadu ili wasiharibu mazao yao ikiwa ni pamoja na suala kujua faida ya kupima afya ya udongo kabla ya kuingia kwenye kilimo hicho.
WAWEKEZAJI,MKULIMA
Wakizungumza kwa nyakati tofauti faida ya ardhi katika matumizi ya kilimo wamesema kuwa ardhi wanaitumia katika mambo mbalimbali yakiwamo kutumia katika kilimo ambacho kinawapatia mazao ya chakula na biashara pamoja na kutumia hati miliki kupata mikopo.
Mkazi wa Chamwino,David Mwaka, mkulima wa Kilimo bustani (Hotculture), amesema kuwa ardhi inafaida nyingi mtu akiwa na hati miliki atapata mkopo wa kuweza kuendeleza masuala mengine ya kimaendeleo.
"Nina ardhi kubwa nimechimba kisima cha maji na nafanya kilimo cha umwagiliaji, ardhi natumia katika kilimo naweza kulima kuanzia Januari hadi Disemba," amesema mkulima huyo.
Mwaka amewataka wakulima wengine na vijana kuthamini ardhi kwa kuwa ndiyo inayoweza kumnufaisha mtu kwa haraka endapo atazingatia kanuni za kilimo.
Ameongeza kuwa katika kuongeza uzalishaji wake huwa anatumia mbolea aina tofauti tofauti kulinaga na bei za sokoni za mbolea hizo.
Akizungumzia uelewa wa afya ya udongo katika uzalishaji wake amesema ni muhimu mkulima kufahamu aina ya afya hiyo ya udongo ili aweze kupanda mazao yanayoendana na udogo.
Mwaka amefafanua kuwa upimaji wa udogo kabla kuanza kilimo una leta tija na kwamba baada ya kupata elimu ya afya ya udongo kwa sasa anapanda mazao kulingana na mtaalamu wa udogo anavyomshauri.
"Kwa sasa najua ni aina gani ya zao linalotakiwa kupandwa, unapoingia kwenye kilimo kunahitaji kujiandaa haswa kwani kilimo kinahitaji uwekezaji wa kutosha mbali na matumizi ya mbolea kuna suala la afya ya udongo wataalamu wanasema ili kuweza kufanikiwa lazima upime afya ya udongo,’’ameeleza.
Naye mkazi wa Mpunguzi jijini Janeth Lwabe ambaye ni mkulima amesema ardhi inampatia manufaa kwa kuwa analima mazao ya biashara na ya chakula ambapo anatumia kama chakula na kuuza kwa ajili ya kujipatia fedha za kujikimu na familia.
Akizungumzia changamoto ya migogoro ya mipaka ya ardhi amesema kuwa wamekuwa wakikumbana na migogoro hiyo katika mashamba yao hali inayosababisha kutokuelewana wao kwa wao.
Pia Janeth ameiomba serikali kuwasaidia mblolea ili kuyaboresha mashamba yao kwa kuwa yamekosa rutuba.
Mkuu wa Maabara Kuu ya Udongo Tanzania, Mkoa wa Tanga kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Mlingano Dk.Kobusinge Aloys ameeleza kwamba kabla ya kuanza uwekezaji wa kilimo mwekezaji, mkulima anatakiwa kupeleka sampuli ya udongo katika maabara hiyo ili kuangalia Afya ya udongo kwenye shamba lake.
Amesema kuwa Shamba linaweza kuwa kubwa au dogo lakini ndani ya shamba hilo kuna aina tofauti ya udongo linaweza likawa na udongo wa kichanga au mfinyanzi hivyo wanawashauri sampuli ichukuliwe na mtu sahihi anayefahamu vizuri masuala ya udongo," amesema.
Ameongeza kuwa vitu vingine wanavyoangalia katika afya ya udongo ni pamoja na chimvi na tindikali.
MBINU ZA UCHUKUAJI WA SAMPULI YA UDONGO
Mkuu huyo wa maabara amesema kuwa uchukuaji wa sampuli za udongo unahitaji mtu sahihi anayeweza kuchukua sampuli hiyo ambayo ni wakilishi kwa shamba zima.
Akizungimzia Mkuu huyo wa Maabara amesema wanashauri sampuli ya udongo ili iweze kuchukuliwa vema ni vizuri kupata watu sahihi wa kuchukua udongo huo kwa lengo la kuepuka kuathiri majibu ya mwisho yanayopatikana katika uhakiki wa vipimo.
Dk. Kobusinge amefafanua kuwa wanaangalia hali ya udongo je virutubisho vipo chini, juu au vipo sahihi kulingana na zao husika linalotakiwa kulimwa katika shamba hilo.
"Kwa kuwa hii ni kazi ya serikali mwekezaji, mkulima atapatiwa namba ya kulipia baada ya kulipia sampuli ya udongo wake itafanyiwa uhakiki na kupatiwa majibu pamoja na ushauri ni nini afanye ndani ya shamba lake kulingana na mahojiano ambayo tumefanya na mwekezaji na kugundua anahitaji kufanya kilimo cha aina gani," ameeleza.
MKURUGENZI WA TARI
Akitoa maelezo kuhusu taasisi hiyo Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dk. Geofrey Mkamilo ameeleza kuwa jambo la kwanza mwekezaji lazima ajue kilimo ni Sayansi kuanzia afya ya udongo sio mtu yeyote anaweza kulima.
"Tunawatu mahiri wa masuala ya udongo,mwekezaji akishajua afya ya udongo itasaidia kujua kama anaweka mbolea ya aina gani, kiasi gani, kwa wakati gani, kwa mpangilio gani," amesema Dk. Mkamilo.
Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa wana vituo mahiri 17,nchi nzima vya mazoa mahiri ya kimkakati kwa lengo la kuhakikisha Tanzania inakuwa na chakula cha kujitosheleza pia kilimo kiweze kuchangia uchumi wa nchi.
TFRA
Dk. Stephan Ngailo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania ( TFRA), amesema kuwa Tanzania ni kitovu cha mbolea katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Ameongeza kuwa soko la mbolea ni kubwa hapa nchini na hata nchi zinazoizunguka Tanzania.
"Idadi ya watu inaongezeka na ardhi inabaki pale pale lazima tuongeze tija kwa kuzingatia kanuni bora ikiwamo matumizi sahihi ya mbolea," amesema.
Ameongeza kuwa TFRA imeanzishwa mwaka chini ya Sheria Namba 9 ya mwaka 2009 ikiwa na jukumu la kusimamia tasnia ya mbolea nchini pamoja na majukumu mengine ni kuhakikisha mbolea hiyo inayotumika, inayoingia, inayosafirishwa nje ya nchi katika ubora na vigezo vya biashara vinazingatiwa
0 Comments