DK.GWAJIMA: TAKWIMU ZINAONESHA HALI YA UKEKETAJI NCHINI BADO NI TATIZO


Na Asha Mwakyonde, Dodoma

TAKWIMU zinaonyesha  ukeketaji nchini bado ni tatizo hali inayotokana na baadhi ya jamii zetu kuendelea kukumbatia mila na desturi zenye madhara na kuwadhalilisha watoto wa kike. 

Pia amewataka  wa Mikoa na Wilaya  kuhakikisha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji dhidi ya Wanawake na watoto wa kike Duniani yanafanyika ngazi zote kwa kuandaa Mdahalo wa Wadau wanaotekeleza shughuli za kutokomeza ukeketaji nchini na kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya ukeketaji kwa njia ya mikutano ya hadhara, vikao pamoja na maandamano. 

Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Waziri wa Maendeleo ya Jamii , Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dk. Dorothy Gwajima wakati akizungumzia kuelekea katika Maadhimisho hayo Februari 6, mwaka huu ambapo  kaulimbiu ya kimataifa ya kupinga ukeketaji Duniani ni “Wanaume na Wavulana; Tushiriki Kupinga Mila na Desturi zenye Madhara ili kutokomeza Ukeketaji”. 

Dk. Gwajima ameeleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na Wadau inaendelea na jitihada za kukabiliana na vitendo vya ukeketaji kupitia mipango na mikakati iliyowekwa ikiwemo kutunga na kufanya marekebisho ya sheria na sera mbalimbali za nchi.

"Kauli mbiu hii inahimiza ushiriki wa wanaume na wavulana katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukeketaji ambayo ni kinyume cha Sheria na kinyume cha haki za binadamu," amesema  Dk. Gwajima.

Amesema  kaulimbiu inatambua umuhimu wa wanaume na wavulana katika kushawishi  wanawake na watoto wa kike  kutotamani kufanyiwa  ukeketaji. Kwa ajili hiyo mitazamo ya wanaume inatakiwa kubadilika kwanza ndipo jitihada za kupinga ukeketaji zinaweza kufanikiwa.


Waziri huyo amesema mwaka huu 2023 maadhimisho hayo yatafanyika katika ngazi ya Mikoa, kulingana na mazingira yao na kiwango cha hali ya ukeketeji.

Dk. Gwajima  ameeleza kuwa maadhimisho hayo yalilenga kuhamasisha jamii kukomesha vitendo vya ukeketaji kwa wanawake na watoto na kuwashirikisha Wanaume na Wavulana kushiriki kupinga Mila na Desturi zenye madhara ili kutokomeza Ukeketaji. 

Amefafanua kuwa madhara ya Ukeketaji ni pamoja na kupoteza damu nyingi na kusababisha vifo, maambukizi ya VVU/UKIMWI na kusababisha matatizo wakati wa kujifungua. 

Waziri huyo amesema madhara  mengine ni watoto kushindwa kuhudhuria shule,kwenye vipindi kwa muda mrefu na hivyo kuzorotesha maendeleo yao kielimu wakati wa kukeketwa.

" Kupitia maadhimisho haya wanaume na wavulana wanaweza kujipima na kukataa ukeketaji kwa wanawake na watoto wa kike na kuona ni kwa namna gani wanaweza kusaidia kupunguza na kukabiliana na vitendo hivyo na kutatua changamoto zinazojitokeza katika mapambano haya na kubuni mikakati mipya,"amesema.


Kwa mujibu wa Dk. Gwajima, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1977 inasisitiza usawa na heshima kwa binadamu wote, kutambua na kuthamini utu wa mtu pamoja na kuhakikisha haki mbele ya sheria.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Watoto Sehemu ya Familia Asha Shame amesema Tanzania ina asilimia 10 ya vitendo vya ukeketaji  huku akiitaja  mikoa inayoongoza kwa vitendo hivyo kuwa ni Manyara  asilimia 58,Dodoma  asilimia 47,Arusha  asilimia 41,Mara  asilimia 32 na Singida  asilimia 31.

Naye Mratibu wa Kutokomeza ukeketeaji Tanzania Denis Mose mikoa inayoongoza kwa kuwa na wanaume wengi ambao hawajaingia tohara baada ya kampeni iliyofanywa na Serikali kwa kushirikiana na mashiriki mbalimbali imesaidia mikoa ya Njombe,Iringa,Singida na Tabora ambapo  Wanaume wengi kuingia tohara hiyo.

Baraza la Umoja wa Mataifa liliidhinisha kufanyika kwa Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji kwa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kwa lengo la kutokomeza vitendo vya ukeketaji kwa wanawake na watoto wa kike duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 06 Februari. 

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU