MFUKO WA NSSF UMELIPA ZAIDI YA BILIONI 350 KWA WASTAAFU NA WANUFAIKA


Na Asha Mwakyonde, Dodoma

KATIKA nusu ya mwaka wa fedha iliyoishia Disemba 2022, Mfuko waTaifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF),ulilipa mafao ya shilingi bilioni 350.7 kwa wanachama, wastaafu na wanufaika wengine wapatao 80,3 ambapo malipo hayo yanajumuisha shilingi bilioni 2.6 zilizolipwa kwa watumishi 183 waliofutiwa ajira kwa kukosa vyeti halali baada ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuelekeza watumishi hao kulipwa mafao ya michango waliyochangia katika kipindi cha ajira zao.    

Pia katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 2023, Mfuko  huo unatarajia kulipa mafao yenye thamani ya shilingi bilioni 769.3 ambayo ni ongezeko la asilimia 17 ukilinganisha na shilingi bilioni 659.8 zilizolipwa katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2022. 

Akizingumza jijini Dodoma Februari 8,2023 Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Masha Mshomba wakati wa Utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mfuko huo na mwelekeo wa utendaji katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 amesema 
 katika eneo hili la mafao, amemshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia ombi la vyama vya wafanyakazi (kupitia TUCTA) la kuja na kikokotoo kipya kwa ajili ya manufaa ya wastaafu wetu ambacho kilianza kutumika Julai 2022.

Amesema kuwa sasa wastaafu wanapokea mkupuo wa awali wa asilimia 33 ukilinganisha na asilimia 25 ambayo wastaafu wa NSSF walikuwa wanapata na kwamba  jambo la muhimu ni kikokotoo hicho  kinazingatia uendelevu wa mifuko ya hifadhi ya jamii. 

Mkurugenzi huyo akizungumzia uwekezaji mpya  wa NSSF ameeleza kuwa katika nusu ya mwaka iliyoishia Disemba 2022, Mfuko uliwekeza shilingi bilioni 483 katika uwekezaji mpya ikujumuisha hatifungani, amana za mabenki, dhamana (corporate bonds) kwa makampuni (NMB, TMRC na NBC), miradi ya ujenzi na uwekezaji katika kiwanda cha sukari Mkulazi.

"Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 246 sawa na asilimia 51 ziliwekezwa katika hati fungani za Serikali. Eneo hili ni salama, lenye faida kwa Mfuko na taifa kwa ujumla kwa kuwa fedha hizi zinatumiwa na Serikali kama fedha za ndani kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo," ameeleza.


Ameongeza kuwa malipo ya kodi 
Katika nusu ya mwaka iliyoishia Desemba 2022, Mfuko ulilipa kodi Serikalini kiasi cha shilingi bilioni 77.9, kodi hiyo  inapolipwa Serikalini inaenda kuwahudumia wananchi kupitia huduma mbalimbali za jamii kama vile afya, elimu, maji na miundombinu. 

Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa ongezeko la wanachama kutokana na Mkakati wa Serikali wa kuvutia wawekezaji serikali imetekeleza mikakakati mbalimbali ya kuvutia wawekezaji wakubwa ikiwa ni pamoja na kupitia maonesho ya filamu ya The Royal Tour. 


Amesema  mikakati hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha kuwa miradi mikubwa ya kimkakati kama vile ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere, Nyanzaga Goldmine, Kiwanda cha mbolea Intracom, Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato, Mgodi wa Uchimbaji wa Madini ya Nikeli (Tembo) uliopo Ngara, Daraja la Kigongo-Busisi Mwanza, kiwanda cha Sukari cha Bagamoyo, mradi wa umeme wa Rusumo na mradi wa reli ya kisasa ya SGR inakamilika. 

"Miradi hii pekee imechangia takribani wanachama wapya 33,066 na kwa ujumla mkakati huu wa Serikali umechangia katika ongezeko la wanachama na michango inayokusanywa na Mfuko,"amesema.

Amesema kutokana na juhudi mbalimbali za Serikali kuvutia uwekezaji na kufungua fursa mpya za biashara, wastani wa makusanyo ya michango kwa mwezi imeongezeka na kufikia shilingi bilioni 134 kutoka wastani wa shilingi bilioni 118 kwa mwezi katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2022. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 14. 

Aidha Mkurugenzi huyo ametoa  rai kwa Waajiri wote nchini kuzingatia sheria za kazi na ajira na kutekeleza jukumu la kuwasilisha michango ya watumishi wao kwa mujibu wa sheria itakayowezesha ulipaji wa mafao kufanyika kwa wakati. 


Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI