📍Ahidi Mabadiliko Makubwa kwa Wafanyakazi na Wastaafu
Na Asha Mwakyonde, DODOMA
KATIKA mwendelezo wa mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, Mgombea Urais wa Chama cha Kijamii (CCK), Bw. David Mwaijojele, amejitokeza rasmi kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mgombea huyo akiwa na mgombea mwenza wake, Masoud Ali Abdalla,wamekabidhiwa fomu hizo na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC),huku wakiahidi mageuzi makubwa katika sekta ya ajira, ustawi wa wafanyakazi, na maisha ya wastaafu endapo watapewa ridhaa ya kuongoza nchi.
Zoezi la uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi ya Rais na Makamu wa Rais nchini limeendelea katika Ofisi za Tume hiyo ambapo mgombea wa kumi hadi sasa, Mwaijojele kutoka CCK, amechukua kuchukua fomu hizo akiwa na mgombea mwenza wake, Abdalla ambazo wamekabidhiwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukamilisha zoezi hilo, Mwaijojele amesema kuwa chama chake kina vipaumbele mbalimbali vya kuwaletea wananchi maendeleo, alivitaja baadhi kuwa ni kilimo cha kisasa, elimu bora, huduma bora za afya, ajira kwa vijana na kuboresha maisha ya wastaafu.
“Tuna vipaumbele vingi, lakini huu si wakati wa kunadi sera. Tutafanya hivyo baada ya kuteuliwa rasmi na Tume,” alisema Mwaijojele.
Ameongeza kuwa endapo watachaguliwa kuongoza nchi, serikali yao italipa kipaumbele suala la ajira na maslahi ya wastaafu, akisema wafanyakazi wengi kwa sasa wanaogopa kustaafu kutokana na mazingira magumu ya maisha.
“Sisi CCK tunayo mikakati madhubuti ya kuandaa mazingira bora kwa wastaafu ili vijana wachukue nafasi hizo kwa ujasiri,” amesema.
Mwaijojele ameeleza kuwa serikali ya CCK itaweka utaratibu wa kuwajengea wafanyakazi nyumba wakati bado wako kazini kwa kutumia kodi zitakazokatwa kwa utaratibu maalum.
Aidha, ameahidi kuwa serikali yao itakuwa na mikakati ya kuwawezesha wananchi wa kawaida, wajasiriamali wadogo, wachimbaji madini, waandishi wa habari na wafanyabiashara kwa kuweka mazingira mazuri ya kujiendeleza kiuchumi, ikiwemo kusaidia katika kupata maeneo ya biashara na mitaji midogo.
“Tunazo sera nzuri sana, tuna ilani bora kuliko zote hata kuliko ya CCM,” alisema kwa kujiamini," ameeleza Mwaijojele.
Aidha ameishukuru INEC kwa usimamizi mzuri wa mchakato wa uchaguzi hadi sasa, akisema wamekuwa wakishirikiana kwa karibu katika kila hatua.
0 Comments