WADAU WA KILIMO WATAKIWA KUUELEWA NA KUUTEKELEZA MPANGO MKUU WA KILIMO - ATO


Na Asha Mwakyonde, DODOMA

KIONGOZI wa Sekta ya Mifugo na Uvuvi kutoka Ofisi ya Mageuzi ya Kilimo (ATO), Joseph Temu, ametoa wito kwa wadau wote wanaoshiriki katika mnyororo wa thamani ya mazao ya kilimo kuelewa kwa kina Mpango Mkuu wa Kilimo wa Tanzania, ujulikanao kama Tanzania Agriculture Master Plan, pamoja na nafasi zao katika utekelezaji wake.

Akizungumza hivi karibuni katika Maonesho ya 32 ya Kilimo ya mwaka 2025, Temu amesema kuwa utekelezaji wa mpango huo ni sehemu ya kutimiza Dira ya Taifa ya Kilimo. 

Amebainisha kuwa dira hiyo iliandaliwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wa sekta hiyo, wakiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi, vyama vya ushirika, sekta binafsi, serikali pamoja na wabia wa maendeleo.

Ameongeza kuwa mpango huo umebeba maono ya pamoja ya kila mdau, na kwamba katika maandalizi yake, ulifanyika uchambuzi wa kina uliosaidia kubaini malengo mahususi yanayolengwa kufikiwa ifikapo mwaka 2050.

Temu ameeleza kuwa lengo kuu la dira ya 2050 ni kulifikisha Taifa kwenye uchumi wa kati wa juu, ambapo sekta ya kilimo inatarajiwa kuwa mhimili mkuu wa mabadiliko hayo.

“Sekta ya kilimo ina waajiriwa wengi zaidi nchini, ambapo zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania wanaitegemea. Ikiwa tutaweza kuwawezesha kuongeza tija na kipato, basi kufikia lengo la Taifa litakuwa rahisi zaidi, tofauti na kutegemea sekta chache zenye mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa lakini zenye waajiriwa wachache,” amesema Temu.

Amesisitiza kuwa mpango huu wa Mageuzi ya Kilimo (Agriculture Transformation Master Plan) ni kioo kinachotafakari dira ya mwaka 2050 kwa sekta ya kilimo, na unalenga kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika maendeleo ya kiuchumi.

Ofisi ya Mageuzi ya Kilimo (ATO) ni taasisi iliyoundwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Kilimo na wadau wa maendeleo. Lengo kuu la ofisi hiyo ni kuandaa, kuratibu na kuwezesha utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Mageuzi ya Kilimo nchini.

Kwa upande wake, Mtaalamu kutoka ATO, Francis Ndumbaro, amesema kuwa kimsingi wakulima, wafugaji, na wavuvi ndio wadau wakuu katika mnyororo mzima wa uzalishaji na biashara ya Mpango Mkuu (Master Plan).

"Ili tuweze kufikia malengo haya, wakulima wanapaswa kuelekeza nguvu zao katika mpango huu kwa kuwa wao ndio msingi mkuu; kisha wadau wengine watafuata," alisema mtaalamu huyo.

Ameongeza kuwa ili wakulima waweze kufanikiwa, wanapaswa kuwa na mkakati madhubuti, kwani wana mazao na mifugo ya aina mbalimbali ndani ya mpango huu. Hivyo, aliwashauri kuweka vipaumbele badala ya kulima au kufuga kila kitu kwa wakati mmoja.

Ndumbaro amesema kuwa rasilimali walizonazo fedha na nguvu kazi ni ndogo, hivyo ni muhimu kuchagua eneo moja lenye tija zaidi litakalowasukuma kufikia malengo yao kwa ufanisi.

Post a Comment

0 Comments

WALIMBWENDE WA MISS GRAND TANZANIA WAFANYA ZIARA YA MAFUNZO HIFADHI YA PANDE