Daktari Bingwa Mbobezi wa Magonjwa ya Upasuaji Mifupa kwa Watoto kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI),Dk. Bryson Mcharo.
Na Asha Mwakyonde
MIFUPA laini ni ugonjwa ambao unawapata watoto wenye umri wa kuzaliwa na hata katika umri wa miaka 10 na kuendelea.
Kwa kawaida mtoto anazaliwa na tatizo hilo la kuvunjika vunjika mifupa yake kwa sababu ya ulaini huo.
Akizungumzia sababu za mtoto kuzaliwa na ugonjwa wa mifupa laini Daktari Bingwa Mbobezi wa Magonjwa ya Upasuaji Mifupa kwa Watoto kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) ,Dk. Bryson Mcharo anasema kinachosababisha ni ukosefu wa aina ya Protini inayoitwa Collagen type 1.
Dk. Mcharo anasema ni aina ya Protini ambayo inahitajika kuwa na mifupa ambayo ni imara na kwamba sababu kubwa zinazoonekana ni za kurithishana.
"Mtu anapata ugonjwa huu kutoka kwa wazazi wake kwa muundo mpya wa mabadiliko ya aina fulani," anasema Dk. Mcharo.
DALILI ZAKE
Dk. Mcharo anafafanua kuwa dalili za ugonjwa huo ni watoto kuvunjika vunjika mifupa mara nyingi, kuwa na rangi ya bluu sehemu ambazo zinatakiwa kuwa kawaida mfano weupe wa jicho unakuwa wa bluu.
"Lakini hata sehemu nyingine za mwili zinazotakiwa kuwa na weupe zina za bluu pia watoto kuwa na kimo kifupi," anasema daktari huyo.
Daktari huyo ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Watoto katika taasisi hiyo anasema watoto hao wanaweza kuwa na viungo ambavyo havijanyooka.
Anasema wanaweza kugundua tatizo kupitia dalili na kuvunjika vunjika vunjika na kwamba inawezekana mtoto amevunjika zaidi ya mara tatu.
" Katika kugundua tatizo tunaweza kutumia kipimo cha vinasaba (DNA), Lab Invistgation DNA Test, " anasema.
KUFIKA MOI
Dk.Mcharo anasema watoto wengine wanaweza kufikishwa MOI wakiwa na viungo ambavyo havijanyooka.
" Wapo wengine wanaweza kuja na migongo ambayo imepinda na wengine wanakuja na sababu ya kushindwa kutembea kwa kuwa wamevunjika vunjika,"anaeleza Dk. Mcharo.
KUHUSU UELEWA
Dkatari huyo anaongeza kuwa watoto wenye ugonjwa wa mifupa laini wanakuwa na akili za kawaida darasani kama ilivyo kwa wengine.
" Lakini tatizo kubwa linakuwa kwenye kutembea au kushindwa kutembea kwa sababu ya kuvunjika vunjika ,," anesema.
Anaeleza kuwa watoto hao wanakuwa na viungo laini na wakati mwingine vinashindwa kuhimili uzito wa ntoto.
UKUBWA WA TATIZO
Daktari huyo Mbobezi anaongeza kwa majarida ambayo yapo yanaonyesha kuwa Kila watu 15,000 mmoja anatatizo la ugonjwa wa mifupa laini na kwmba inaonyesha tatizo ni kubwa kiasi gani.
Anasema kwa upande wa MOI wanapata watoto wenye ugonjwa hou wawili kwa mwezi na kwamba mbaya zaidi wanafiki wakiwa katika hatua ambayo wamevunjika vunjika.
" Mbaya zaidi unakuta wengi hawajawahi kutembea wanapo kuja katika hali hiyo kidogo inafanya matibabu kuwa zaidi au ugumu na matibabu yake huwa yanaigharimu serikali, "anaongeza:
Kama wangekuwa wanakuja mapema tungeweza kuzuia kuendelea kuvunjika vunjika," anasema Dkt. Mcharo.
MATIBABU YAKE
Anaeleza kuwa mara nyingi watoto hao wanapowagundua mwanzoni Kwanza kabisa wanatoa ushauri kwa wazazi wanatakiwa kuwaangalia vipi ili wasiendelee kuvunjika.
Dkatari huyo anaongeza kuwa kwa wale ambao wapo katika hatua ambazo tayari wameshavunjika wanawasaudia kwa kuwawekea vyuma ndani ya mifupa ili wasiendelee kuvunjika vunjika.
" Kwa wengi ambao tayari tumeshawawekea vyuma hawaji tena hospitalini mara kwa mara wangi wanakuwa wapo vizuri," anaeleza daktari huyo.
WITO KWA JAMII
Dk.Mcharo anawataka wazazi kuwa na utaratibu wa kuwapeleka watoto wao kwa madaktari bingwa wa mifupa ili kuweza kugundua ugonjwa wa mifupa laini pindi wanapozaliwa.
Daktari huyo Mbobezi, anasema kwa sasa Watanzania hawawezi kuliepuka tatizo hilo la ugonjwa wa mifupa laini.
Dk.Mcharo anasema kwa nchi ambazo zimeendelea akizaliwa mtoto anapelekwa kwa daktari bingwa wa mifupa wa watoto lengo ni kugundua tatizo na kuanza kupatiwa matibabu mapema.
"Bahati nzuri kwa sasa Tanzania ina madaktari bingwa wa mifupa wa watoto. Ni vizuri wazazi wakaanza kumpeleka mtoto kwa daktari wa mifupa pindi anapozaliwa hasa wanapoona dalili ambazo sio sahihi," anasema.
Anasema tatizo hilo lipo na kwamba lina athiri watoto, takwimu zinaonyesha kati ya watu 15,000 mmoja anazaliwa na ugonjwa wa mifupa laini.
Dk.Mcharo anasema kuwa katika taasisi hiyo kuna madaktari wabobezi na kwamba wapo baadhi ya watoto walifika wakiwa hawajaanza kutembea baada ya kupatiwa huduma wanatembea.
" Watu ambao wanahusika na kutoa huduma za afya wanapo waona watoto hawa hasa wale wakunga wanapowazalisha kwani dalili nyingi zinaonekana mwanzoni wawashauri wazazi," anasema Dk.Mcharo.
0 Comments