Na Anastazia Anyimike
MGOMBEA wa kiti cha rais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Rais Samia Suluhu Hassan amesema kila ahadi iliyowekwa kwenye ilani ya uchaguzi inakwenda kutekelezwa kwani wanajua fedha za kutekeleza zinatoka wapi.
Akiomba ridhaa ya wananchi, Same mkoani Kilimanjaro, Samia alisema: " kila tulichokiweka mule (ndani ya Ilani) tunajua fedha yake ya utekelezaji inatoka wapi."
"Lakini nataka niwaambie lingine tumeongeza makusanyo ya mapato.
Na tunaendelea kuongeza makusanyo ya mapato ndani ya nchi yetu kuepuka nyanyaso za mikopo kuepuka nyanyaso za misaada. Tunajua hakika fedha zinatoka wapi. Tutakopa ndiyo lakini mikopo ambayo itaheshimu uhuru wa nchi yetu ndiyo tutakayokopa."
Samia amesema faraja yake ni kutokana na kuweza kutimiza mradi ambao marehemu Waziri Mkuu Mstaafu Cliopa Msuya ambayo ilikuwa ni mradi wake wa kufa na kupona.
"Alinifuata na akaniomba miradi miwili mradi mmoja maji safi Mwanga - Korogwe na mradi wa pili wa barabara ya Msuya bypass."
"Faraja yangu ni kwamba miradi yote miwili nimeweza kuifanya ameiona kabla ya Mungu hajamchukua kwa hiyo nawashukuru wanamwanga. Niseme kwamba kwenye maji tumeweza kupandisha asilimia ya upatikanaji maji kutoa 77.5 mwaka 2023 hadi 81.9 mwaka jana."
Amesema kuwa miradi 26 imefanyika hapa kwa bilioni 54.2 na mradi wa Same Mwanga Korogwe peke yake una bilioni 304 kwa hiyo ni mradi mkubwa sana.
"Tumetekeleza mradi huu kwa awamu ya kwanza ambayo tayari maji yameanza kupatikana. Na awamu ya pili ni kwenye maenwo yaliyobaki Same baadhi na kule Korogwe."
"Kama nilivyomuahidi marehemu Mzee Msuya tutakwenda kuukamilisha mradi huu sambamba na ile barabara ya Msuya bypass."
"Tumejenga minara sita ya simu katika Tarafa ya Jipendea ili kuimarisha mawasiliano ya simu na kuwawezesha wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi. Sasa hivi mambo yote kwenye simu, kununua kwenye simu kutangaza biashara kwenye simu lazima tuhakikishw network inapatikana kila mahali. "
0 Comments