Morogoro,
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), imeendelea kuimarisha mafanikio yake ya kitaasisi kupitia ushirikiano madhubuti kati ya uongozi na wafanyakazi, hali iliyodhihirishwa katika kipindi cha miaka mitano ya Baraza la Sita la Wafanyakazi lililomaliza muda wake wa kuhudumu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha mwisho cha Baraza hilo kilichofanyika Februari 5, 2026 mkoani Morogoro, Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dk. Adam Fimbo, aliwapongeza wajumbe wa baraza hilo kwa mchango wao mkubwa katika kuleta mafanikio yaliyopatikana ndani ya taasisi hiyo, akisisitiza kuwa mafanikio hayo yametokana na mahusiano mazuri kati ya uongozi na wafanyakazi kupitia ushirikishwaji katika maamuzi makubwa ya kitaasisi.
Dk. Fimbo amesema kuwa katika kipindi cha uongozi wa Baraza la Sita, TMDA imefanikiwa kukamilisha miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa jengo la ofisi ya Makao Makuu jijini Dodoma, nyumba za taasisi katika vituo vya mipaka vya Namanga na Tarakea, pamoja na ujenzi wa tanuru la kisasa la kuteketeza bidhaa duni na bandia kwa lengo la kulinda afya ya jamii.
Aidha, ameongeza kuwa TMDA imefikia ngazi ya tatu ya ukomavu wa mifumo ya udhibiti wa dawa ya Shirika la Afya Duniani (WHO Maturity Level 3 ML3), hatua iliyoiweka Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kufikia hadhi hiyo. Pia, maabara za TMDA zimetambuliwa na WHO kuwa miongoni mwa maabara bora duniani, huku TMDA ikiteuliwa kuwa Kituo cha Umahiri cha udhibiti wa dawa, chanjo na utoaji wa mafunzo ya kiudhibiti barani Afrika.
Katika hatua nyingine, Dk. Fimbo amesema Baraza la Sita la Wafanyakazi limechangia kwa kiasi kikubwa kuweka mazingira wezeshi ya uanzishaji na uendelezaji wa viwanda vya dawa nchini, ambapo hadi sasa kuna viwanda 19 vya dawa za binadamu, viwanda 2 vya dawa za mifugo na viwanda 41 vya vifaa tiba.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Ofisi ya TUGHE Makao Makuu, Wakili Mwanaidi Mgowa, ameupogeza uongozi wa TMDA kwa kuwa na Baraza la Wafanyakazi la mfano wa kuigwa, akieleza kuwa limekuwa kielelezo kwa mabaraza mengine nchini. Aidha, aliwahimiza wajumbe wa TUGHE kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi wa ngazi ya Mkoa na Taifa unaotarajiwa kufanyika ndani ya mwaka 2026.
Akitoa salamu kwa niaba ya Kamishna wa Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano, Peter Sembuyagi aliipongeza TMDA kwa kufikia mafanikio makubwa yaliyotokana na utekelezaji wa dhana ya ushirikishwaji mahala pa kazi, akisisitiza kuwa ni takwa la kisheria linalopaswa kuendelezwa katika taasisi zote.
Baraza la Wafanyakazi wa TMDA huundwa kwa kipindi cha miaka mitano na linajumuisha Menejimenti, wajumbe wa TUGHE pamoja na wawakilishi kutoka ofisi zote za kanda, ambapo hukutana mara mbili kwa mwaka kujadili masuala makubwa ya kitaasisi kama sehemu ya kuwashirikisha watumishi katika ngazi ya maamuzi.




.jpg)

0 Comments