TEHAMA YACHOCHEA UCHUMI WA KIDIJITALI NDANI YA SIKU 100


 Na Asha Mwakyonde, DODOMA 

SERIKALI kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imetekeleza kwa mafanikio ahadi za siku 100 zilizoelekezwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, katika sekta ya mawasiliano na TEHAMA, hali inayothibitisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kujenga uchumi wa kidijitali unaojumuisha wananchi wote.

Hayo yalisemwa jana jijini hapa na Waziri wa Wizara hiyo Angellah Kairuki wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa ahadi za siku 100 zilizotolewa na Rais Dk Samia 

alisema sekta ya TEHAMA ni mhimili wa maendeleo ya Taifa kwa kuwa inagusa sekta zote, na ndiyo msingi wa mapinduzi ya kidijitali yanayolenga kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kidijitali unaoendeshwa na teknolojia.

Waziri Kairuki alisema kati ya ahadi 13 zilizotolewa na Rais Samia wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ahadi tatu ziligusa moja kwa moja Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, na zote zimeanza kutekelezwa ndani ya muda uliopangwa, hatua iliyoongeza imani ya wananchi kwa uongozi wa Rais Samia katika kipindi cha awamu ya pili.

Katika utekelezaji wa ahadi ya kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa kampuni changa, Waziri Kairuki alisema Serikali imetenga Shilingi bilioni 5 kwa ajili ya kusaidia kampuni changa 50 za TEHAMA kupitia mikopo yenye riba nafuu itakayotolewa na benki za biashara, hatua inayotarajiwa kuongeza ajira, kukuza bunifu na kuchochea ukuaji wa biashara zinazoendeshwa na vijana.

"Wizara imeanza taratibu za kuanzisha Mfuko wa Kitaifa wa Uwezeshaji wa Kampuni Changa za TEHAMA pamoja na kukamilisha rasimu ya Sera ya Kampuni Changa ya Mwaka 2026, inayolenga kuweka mazingira rafiki ya biashara, kuongeza upatikanaji wa mitaji, kuvutia uwekezaji na kukuza ajira kwa vijana nchini," alisema.

Katika eneo la ujuzi na rasilimali watu, Waziri Kairuki alisema Serikali imeanza maandalizi ya ujenzi wa Taasisi ya Taifa ya Teknolojia ya Kidijitali (NDTI) jijini Dodoma, itakayotoa mafunzo ya teknolojia zinazoibukia kama Akili Unde, Usalama wa Mtandao na Uchambuzi wa Takwimu, sambamba na ushirikiano na vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi.

Akizungumzia kuhusu uwajibikaji wa viongozi na upatikanaji wa huduma kwa wananchi, Waziri alieleza kuwa Wizara imeunganisha taasisi 800 za umma kwenye Mtandao wa Serikali (GovNet), imeendeleza mifumo ya kidijitali ya kupokea na kushughulikia kero za wananchi, na ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mifumo ya Tembo Portal na Jamii Portal itakayozinduliwa rasmi Aprili 2026.

Aliongeza kuwa katika kipindi hicho cha siku 100, sekta ya mawasiliano imeendelea kukua kwa kasi ambapo laini za simu zimeongezeka hadi kufikia milioni 106.9, watumiaji wa intaneti milioni 58.1 na watumiaji wa huduma za fedha kwa njia ya simu milioni 76.5, huku Serikali ikiendelea kudhibiti gharama za mawasiliano, kupanua ujenzi wa minara, mkongo wa taifa na kupunguza pengo la kidijitali kati ya mijini na vijijini.


Post a Comment

0 Comments

MARTHA GIDO AKIWA MUNGENI JIJINI DODOMA