Na Asha Mwakyonde, Dodoma
📍Wateja wahimizwa kutoa taarifa pindi haki zao zinapokiukwa.
BAADHI ya wananchi hukaa muda mrefu bila kuunganishiwa maji hata baada ya kulipia gharama, kwa sababu hawajui muda uliowekwa kisheria wala haki yao ya kudai fidia endapo kutakuwa na ucheleweshaji.
Ukosefu wa maji kwa muda mrefu huathiri afya, usafi na shughuli za kiuchumi, hasa pale wananchi wanaposhindwa kudai haki zao kwa wakati.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imeweka bayana viwango vya fidia kwa wateja wa huduma ya maji endapo watoa huduma watashindwa kutekeleza majukumu yao kwa wakati uliopangwa hatua inayolenga kulinda haki za watumiaji wa huduma hiyo nchini.
Akizungumza katika warsha ya siku moja kwa waandishi wa habari ambao ni wanachama wa Chama Cha Waandishi wa habari Mkoa wa Dodoma (DPC), kuhusu udhibiti wa huduma za nishati na maji ambayo imeendaliwa na Mamlaka hiyo.
Kaimu Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Wilfred Mwakalosi, anasema fidia hizo zitatolewa kulingana na aina ya huduma iliyocheleweshwa, kutotolewa ipasavyo, sambamba na muda wa ucheleweshaji.
Kwa mujibu wa EWURA, mteja anayelipia gharama za kuunganishiwa huduma ya maji anapaswa kuunganishiwa ndani ya siku saba za kazi.
Mwakalosi anaeleza kuwa endapo huduma hiyo itachelewa, mtoa huduma atalipa fidia ya shilingi 5,000 kwa kila siku ya kuchelewa, huku ada ya msingi ikiwa shilingi 10,000.
Akizungumzia kuhusu matengenezo au ubadilishaji wa dira ya maji iliyoharibika, anasema EWURA imeelekeza huduma hiyo itolewe ndani ya siku saba za kazi tangu kugundulika, kuripotiwa kwa hitilafu.
"Kushindwa kutekeleza hili kutamfanya mtoa huduma kulipa fidia ya shilingi 5,000 kwa siku, baada ya ada ya shilingi 15,000," anaeleza Mwakalosi.
Aidha, anafafanua kuwa usomaji wa dira ya maji unatakiwa kufanyika angalau mara moja kila mwezi huku akisema kukosekana kwa huduma hiyo kwa wakati kutawajibisha mtoa huduma kulipa fidia ya shilingi 5,000 kwa siku.
KUSITISHA HUDUMA
Akizungumzia kusitisha huduma kimakosa bila ushahidi sahihi, anasema EWURA imeeleza kwamba huduma hiyo inapaswa kurejeshwa ndani ya saa 24 baada ya kupokea taarifa.
"Endapo kutakuwa na ucheleweshaji, mteja atalipwa fidia ya shilingi 5,000 kwa siku, huku ada husika ikiwa shilingi 30,000," amesema.
Anaongeza kuwa kurejeshwa kwa huduma baada ya mteja kulipia deni kunapaswa kufanyika ndani ya saa 24 na kwamba kinyume na hapo, fidia ya shilingi 5,000 kwa siku italipwa.
KUSHUGHULIKIA MALALAMIKO YASIYOHUSIANA NA ANKARA
Mwakalosi anaeleza kuwa katika kushughulikia malalamiko yasiyohusiana na ankara, EWURA imeelekeza uchunguzi na ufumbuzi kukamilika ndani ya siku 15 za kazi, wakati malalamiko yanayohusu bili yanapaswa kushughulikiwa ndani ya siku tano za kazi.
Anaongeza kuwa kushindwa kuzingatia muda huo kutasababisha mtoa huduma kulipa fidia ya shilingi 5,000 kwa siku.
Mwakalosi anasema utekelezaji wa viwango hivyo ni sehemu ya jitihada za EWURA kuhakikisha uwajibikaji, uwazi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
"Nawahimiza wateja kutoa taarifa pindi haki zao zinapokiukwa.
EWURA YAWAKUMBUSHA WATOA HUDUMA ZA MAJITAJA
Anasema Mamlaka hiyo inawakumbusha watoa huduma za majitaka kuzingatia masuala ya afya na usalama kwa kuhakikisha majitaka hayatoki wala kufurika katika makazi ya wananchi, huku ikibainisha fidia itakayolipwa endapo kosa hilo litajitokeza.
Akizungumza kuhusu viwango hivyo, anabainisha kuwa hairuhusiwi majitaka kutoka kwenye mtandao wa mamlaka kufurika ndani ya nyumba au eneo la mteja, kwani hali hiyo ni hatari kwa afya na usalama wa wananchi.
"Kwa mujibu wa EWURA, endapo majitaka yatafurika ndani ya nyumba au eneo la mteja, mtoa huduma atalazimika kulipa fidia ya shilingi 20,000 kwa kila siku ya kuchelewa kurekebisha tatizo hilo, baada ya ada ya msingi ya shilingi 40,000," anasema.
Aidha, anafafanua kuwa ni kosa majitaka kutoka kwenye mtandao wa mamlaka kutiririka, kufurika nje ya mfumo na kuingia katika maeneo ya makazi ya wananchi.
Anasema mtoa huduma atalazimika kulipa fidia ya shilingi 20,000 kwa siku, baada ya ada ya shilingi 30,000.
Mwakalosi anasema hatua hizo zinalenga kulinda afya za wananchi, mazingira pamoja na kuimarisha uwajibikaji kwa watoa huduma za majitaka nchini, huku akiwahimiza wananchi kutoa taarifa mapema pindi changamoto hizo zinapojitokeza.

.jpg)

0 Comments