📍Yatoa Mbegu za Mbaazi tani moja
Na Asha Mwakyonde, DODOMA
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba Hassan Mnyikah ameishukuru Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA),kwa kuwawezesha wakulima wadogo, wakati na Wakubwa kuwapatia mbegu ya zao la mbaazi tani moja kwa bei ambayo ni sawa na bure
Hayo ameyasema leo Januari 6 ,2026 jijini hapa mara baada ya kukabidhiwa mbegu hizo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule katika hafla ambayo imefanyikia katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo ambapo Halmashauri tatu zimenufaika ambazo ni Kongwa, Kondoa na Chemba.
Amesema mbegu hizo watazitumia katika msimu wa mvua zinazoendelea na kuweza kupata mazao kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na mwaka jana na kwamba zao la mbaazi linaimarisha uchumi kwa wanachemba.
Mkurugenzi huyo amefanunua kuwa kiasi hicho cha mbegu za mbaazi kilichopokelewa ni mrejesho wa zoezi la matumizi ya mfumo wa Stakabadhi ghalani huku akisema mwaka uliopita Wilaya ya Chemba waliweza kusimamia vizuri zao hilo kwa asilimia 95 ambapo liliuzwa kupitia mfumo huo wa Stakabadhi ghalani.
"Nipo hapa kwa ajili ya ukamilishaji wa zoezi la upokeaji wa mbegu ambazo zimetolewa na COPRA kwa ajili ya wananchi wanaolima katika Wilaya ya Chemba.Kwanza niishukuru COPRA kwa kuona hili jambo kwa kuzingatia Wilaya ya Chemba ni miongoni mwa Wilaya zinazolima zao la mbaazi kwa kiasi kikubwa," ameeleza.
Aidha ameihakikishia mamalaka hiyo kuwa watazitumia mbegu hizo vizuri ili kuweza kupata mazao kwa wingi kwa kuzingatia maelekezo ya wataalam wa Kilimo ambao wapo kila eneo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa huo amesema mfumo wa Stakabadhi za Ghala ndiyo mwelekeo na njia rasmi ya Serikali katika uuzaji wa mazao ya kilimo nchini.
Ameeleza kuwa kugawa mbegu za mbaazi bure kwa wakulima ni historia mpya kwa Mkoa wa Dodoma, kwani ni mara ya kwanza tukio hilo kufanyika.
“Hii ni historia nyingine ambayo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameivunja katika sekta ya kilimo. Nawapongeza COPRA pamoja na taasisi zote zinazohusika na mfumo wa Stakabadhi za Ghala,” amesema Senyamule.
Naye Mkuu wa Kanda ya Kati kutoka COPRA, Andrew Mgaya, amesema kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo wamekabidhi mbegu hizo huku akimpongeza Mkuu wa Mkoa kwa juhudi zake za kuhakikisha mbaazi na mazao mengine yanaingizwa kwenye mfumo wa Stakabadhi za Ghala.
Mgaya ameeleza kuwa uingizwaji wa mbaazi na mazao mengine katika mfumo huo umeanza kuzaa matunda.

.jpg)
.jpg)
0 Comments