Wizara ya afya imepokea maoni kutoka kwa wadau kuhusu uendeshaji wa mtihani wa awali


 Waziri wa afya Ummy Mwalimu

Na Mwandishi wetu, Dodoma

WIZARA ya Afya  inatambua umuhimu wa mtihani wa awali katika kulinda taaluma ya udaktari na utakuwa 
chachu ya Madaktari Watarajali kuzingatia mafunzo yao na kuwaandaa kufanya vyema kwenye 
mtihani wa baada ya mafunzo kwa vitendo (post-internship examination) ambao utaendelea 
kama kawaida. 

Katika taarifa iliyotolewa jijini Dodoma leo Februari 03 mwaka huu na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Profesa Abel Makubi imesema  Wizara imepokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu uendeshaji wa mtihani wa awali (pre-internship examination),kwa madaktari watarajali walio katika fani ya udaktari,udaktari wa meno na utaalamu wa Afya shirikishi.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Madaktari,Madaktari wa Meno na Wataalamu wa Afya Shirikishi, Sura ya 152 pamoja na Kanuni ya Mafunzo ya Utarajali, Tangazo la Serikali Na. 703 la mwaka 2018.

Hivyo,Waziri wa Afya,  Ummy Mwalimu ,baada ya kushauriana na watalaamu kuhusu utekelezaji bora wa Kanuni za mafunzo hayo, ameamua kufanya yafuatayo.

Mtihani wa awali (pre-internship examination) kwa Madaktari Watarajali uendelee
kufanyika bila kumzuia mtarajali kujiunga na mafunzo ya utarajali.

Matokeo ya mtihani huo yatakuwa sehemu ya matokeo ya mtihani wa mwisho (postinternship examination) unaofanyika mara baada ya mhitimu kumaliza mafunzo yake 
ya utarajali.

Watarajali wote waliofanya mtihani huo wa awali na kushindwa kuendelea na mafunzo 
ya utarajali,Baraza linaelekezwa kuwapa usajili wa muda na kuweka utaratibu 
utakaowezesha kuendelea na mafunzo ya utarajali katika Hospitali mbalimbali. 

Aidha, mtihani wa awali utaendelea kutoa picha ya viwango vya ufundishaji 
katika vyuo vya udaktari na kuendelea kuviboresha kupitia tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU). 

Pia Wizara hiyo  imepokea maoni ya Wanataaluma kuhusu Mafunzo endelevu ya kitaaluma
(Continuing Professional Development) kwa ajili ya kuhuisha leseni, hivyo Baraza lifanye 
tathmini ya gharama na utaratibu unaofanyika sasa mapema iwezekanavyo wakati utekelezaji 
ukiendelea.

Hivyo mafunzo hayo yanalinda ubora na uendelevu wa taaluma ya udaktari na kwamba Wizara itaendelea kupokea maoni na ushauri ili kuendelea kuboresha mafunzo na viwango vya 
taaluma ya udaktari nchini. Utekelezaji wa tamko hili unaanza mara moja.


Post a Comment

0 Comments

KAMATI YA BUNGE SHERIA YAPONGEZA MAENDELEO YA MATUMIZI YA NeST