Na Asha Mwakyonde, Dar es Salaam
MUHITIMU mhitimu wa Shahada ya Uhandisi wa Matengenezo ya Ndege kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Ladislaus Moshi,amebuni na kutengeneza mfumo wa kisasa utakaosaidia kutambua vitu hatarishi vilivyopo katika njia za kutua na kupaa kwa ndege kwenye viwanja vya ndege.
Akizungumza leo Septemba 24,2025 jijini Dar es Salaam katika maonesho ya wahandisi vijana, Moshi amesema kuwa mfumo huo una uwezo wa kugundua na kutoa taarifa kwa haraka kuhusu taka au vitu vyovyote hatarishi vilivyopo katika njia za ndege kutua na kupaa, hivyo kusaidia usalama na kuongeza ufanisi wa shughuli za usafiri wa anga.
“Kawaida ukaguzi wa njia hizi hufanywa na vikosi maalum vya zimamoto ambao hutembea eneo hilo kila asubuhi na jioni kuondoa vihatarishi. Njia hii siyo tu kwamba ni hatarishi kwa usalama, bali pia huleta ucheleweshaji kwa ndege kutua au kupaa, jambo linalosababisha hasara kwa taifa,” amesema Moshi.
Amefafanua kuwa mfumo wake unaweza kupunguza changamoto hizo kwa kutoa taarifa za vitu kama chupa, tairi au hata ndege waliotua bila ruhusa, kwa wakati halisi (real-time), hivyo kuondoa haja ya kusubiri ukaguzi wa mwongozo wa binadamu.
Ameitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kuutumia mfumo huo ili kuongeza mapato ya sekta ya usafiri wa anga na kuboresha huduma kwa wasafiri.
Aidha katika maonesho hayo hayo, mwanafunzi mwingine kutoka NIT, Wandowa Titus anayesomea Shahada ya Sayansi ya Kompyuta (Computer Science), amewasilisha mfumo wa kiteknolojia unaotumia Akili Mnemba (Artificial Intelligence – AI) kuhesabu idadi ya abiria kwenye vituo vya mabasi yaendayo haraka (Mwendokasi).
Wandowa amesema kuwa mfumo huo umetengenezwa mahsusi kukabiliana na changamoto ya msongamano mkubwa wa abiria na ucheleweshaji wa huduma katika vituo vya Mwendokasi jijini Dar es Salaam.
“Kwa kutumia kamera maalum zitakazowekwa kwenye vituo vya mabasi, mfumo huu utaweza kuhesabu idadi ya abiria waliopo na kuelekeza mabasi katika maeneo yenye uhitaji mkubwa kama vile Kimara, Mbezi, Gerezani na Morocco,” amesema Wandowa.
Ameongeza kuwa mfumo huo utasaidia wasimamizi kupanga ratiba bora ya mabasi kulingana na mahitaji ya wakati husika, hivyo kupunguza usumbufu kwa abiria na kuimarisha usimamizi wa huduma za usafiri wa umma.
Amesema iwapo mfumo huo utaendelezwa kwa kushirikiana na mamlaka husika, utasaidia kuboresha kwa kiasi kikubwa huduma za usafiri wa umma jijini Dar es Salaam na kuondoa malalamiko ya ucheleweshaji na msongamano.
0 Comments