TIC YAJIPANGA KUBORESHA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dk. Maduhu Kazi alifafanua jambo

Na Asha Mwakyonde,Dodoma

MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo Cha Uwekezaji Tanzania (TIC),Dk. Maduhu Kazi amesema kituo hicho kinaendelea kupokea wimbi kubwa la wawekezaji na kujipanga kuboresha huduma zao kwa kuwa wanafahamu umuhimu wa uwekezaji wa miradi mahiri.

Pia amesema wamejipanga kutoa huduma za haraka na kuhakikisha miradi yote inapita ili mikataba inayosainiwa iweze kutekelezwa.

Mkurugenzi huyo ameyasema hayo jana jijini hapa wakati wa kutiliana saini mikataba sita ya miradi ya kimkakati na mahiri ambayo ilisainiwa kwa kuzingatia vigezo vinavyotakiwa na vilivyoainishwa na kamati ya Taifa ya Uwekezaji ya (NISCO), ameeleza kuwa TIC imekuwa ikifanya mikutano ya mara kwa mara na viongozi wa taasisi zinazohudumia wawekezaji.

Amesema lengo la mikutano hiyo ni kuhakikisha changamoto mbalimbali zinazowakabili wawekezaji zinatatuliwa kwa wakati.

Dk.Kazi ameongeza kuwa TIC inaendelea na juhudi za kuunganisha mifumo ya Serikali yaani dirisha la pamoja la kuhudumia wawekezaji la Kielektroniki Tanzania (TelW) kwa taasisi zinazotoa huduma kwa wawekezaji  kwa kufanya maboresho ya mifumo.

Amesema mfumo huo ni suluhisho la wawekezaji na kurahisisha upokeaji wa maombi, utoaji wa huduma za vibali,leseni na usajili kwa wawekezaji kwa haraka.

" Lengo la mfumo huu ni kutumika kurahisisha mtiririko wa taarifa Kati ya taasisi zote zilizopo ndani ya kituo yaani OSFC," ameeleza mkurugenzi huyo.

Amefafanua kuwa watahakikisha kituo hicho wanakabiliana na changamoto zote za uwekezaji na kuzitafutia ufumbuzi kwa haraka ili wawekezaji hao waweze kutekeleza miradi yao walioikusudia katika kipindi husika bila kukwamishwa na taasisi zao.

" Tunaipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya kazi kubwa ya kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara,' amesema.




Post a Comment

0 Comments

UTALII NA MADINI ZINACHANGIA KWA PAMOJA KUKUZA UCHUMI WA TAIFA