Na Asha Mwakyonde, Dodoma
WANANCHI wametakiwa kuwa watulivu pindi wanaposubiri katiba mpya kwani suala hilo limepewa muda ili kufanyiwa uboreshaji wa sheria na vipengele mbalimbali vya katiba ndipo utekelezaji wake utapofanyika.
Hayo yamesemwa jana jijini hapa na Naibu waziri wa Katiba,sheria,Geophrey Pinda wakati akizindua magari mapya ya ofisi za Tume ya Haki za Binadamu na utawala Bora.
Pinda amebainisha kuwa maboresho mbalimbali ndani ya katiba yamekuwa ya kifanyika kila mara ili kuhakikisha haki inatendeka na hiyo inaonyesha dhahiri suala la utawala bora kwa serikali ya Tanzania.
Hata hivyo amesisitiza kuwa wamejikita katika utoaji wa elimu kwa wananchi ili kuijua katiba vizuri na ndipo kuruhusu urekebishwaji wake kwani wengi wa wananchi hao hawaijui vizuri katiba inayotumika sasa.
Aidha Pinda ameipongeza Tume ya haki za binadamu na Utawala bora kwa kufanya matumizi sahihi ya fedha walizopewa na serikali kununua magari kama walivyokuwa wameomba hapo awali jambo ambalo linawajengea uaminifu kwa serikali.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na utawala bora Bwana Methew Mwaimu ameishukuru serikali kwa kuendelea kuwasikiliza pindi wanapowahitaji na pia amempongeza Rais Samia Suluhu Hassani kwa kuruhusu mabinti walikosa masomo kutokana na mimba kurejea mashuleni jambo ambalo linaonyesha dhahiri utendaji wa haki za binadamu na utawala bora.
0 Comments